Defense One: Watawala wa Aal-Saud ni watenda jinai na mafisadi
Mtandao wa habari wa Defense One wa nchini Marekani, umeutaja utawala wa Aal-Saud kuwa ni mtenda jinai na wa kifisadi.
Defense One umetoa ripoti hiyo baada ya kufanya uchunguzi wa kina ndani ya utawala wa Aal-Saud na kuandika kuwa, katika kipindi cha nusu karne iliyopita, mfalme wa Saudi Arabia, alikuwa mtekelezaji mkuu wa siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba, fedha nyingi za utawala huo, ziliifanya hata jamii ya kimataifa kufumbia macho hatua za kichokozi na za kufurutu ada za Saudia katika eneo. Mtandao huo umeongeza kuwa, hatua chafu za utawala wa Saudia, ikiwemo ya kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kama vile, al-Qaidah, Taleban, Daesh, Jab'hatu Nusra na mengine kama hayo na pia hatua ya Riyadh ya kuishambulia kijeshi Yemen kwa miezi mingi sasa, imeonyesha wazi kwamba utawala wa Aal-Saud ni mtendajinai na wa kifisadi. Ripoti hiyo ya Defense One sanjari na kufafanua kuwa utawala wa Aal-Saud, umeshindwa hata kuainisha malengo ya nchi hiyo, imeongeza kuwa, Saudia inaongozwa na genge la watu wachache matajiri wa ukoo mmoja wa Aal-Saud ambao, utajiri wao unashabihiana kikamilifu na mtandao wa wahalifu na watendajinai. Aidha mtandao huo wa Defense One wa nchini Marekani umebainisha kuwa, utawala wa ukoo wa Aal-Saudi hauwezi kudumu kwa miaka mingi kwani si mbali utasambaratika, na kwamba juhudi za wanasiasa wa Marekani kwa ajili ya kuuokoa ukoo huo wa kidikteta kunako kusambaratika kwake, zimepitwa na wakati. Hayo yanajiri katika hali ambayo maelfu ya raia wa Yemen wamefanya maandamano katika miji tofauti ya nchi hiyo kupinga mwendelezo wa hujuma za ndege za Saudia na waitifaki wake nchini humo ambapo karibu watu 8000, wameuawa na maelfu ya wengine wengi kujeruhiwa.