Sisitizo la Wapalestina la kuendelea na muqawama
Kwa mara nyingine tena, Wapalestina wametumia mnasaba mwingine uliojitokeza kutangaza uungaji mkono wao kwa muqawama hadi watakapofanikisha malengo yote ya taifa lao. Mara hii wapalestina hao wamesisitiza uungaji mkono wao huo wakati wa maadhimisho ya mwaka wa 16 wa kukumbuka Intifadha ya al Aqsa.
Maadhimisho ya mwaka wa 16 wa Intifadha ya al Aqsa yamefanyika katika mazingira ambayo hali ya Wapalestina inazidi kusikitisha kutokana na kuendelea kuzingirwa kila upande na kukabiliana mikono mitupu na dola pandikizi ambalo limejizatiti kwa silaha za kila aina na linaungwa mkono na madola yote ya kibeberu na vitimbakwiri vyao. Tarehe 28 Septemba ndiyo siku ya kuadhimisha na kukumbuka Intifadha ya Pili ya Wapalestina, maarufu kwa jina la Intifadha ya al Aqsa.
Aliyechochea Intifadha hiyo alikuwa ni nduli Ariel Sharon, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni ambaye aliingia kwa makusudi kwenye eneo la Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani msikiti wa al Aqsa, suala ambalo lilikuwa ni sawa na kulitia najisi eneo hilo takatifu. Ni jambo lisilo na shaka kuwa, Intifadha ya Quds ni muendelezo wa Intifadha mbili zilizotangulia, Intifadha ya al Aqsa na Intifadha ya Mawe za wanamapambano wa Palestina. Tarehe 28 Setemba mwaka 2000, Ariel Sharon, mmoja wa viongozi wakuu wa utawala wa Kizayuni, huku akiwa na kundi kubwa la wanajeshi na maafisa usalama wa Israel aliamua kwa makusudi kuwachokoza Wapalestina kwa kuingia katika eneo la Masjidul Aqswa.
Kitendo hicho cha kijuba na kijeuri ulikuwa ni uvunjaji wa wazi wa heshima ya Kibla hicho cha Kwanza cha Waislamu, na ndio maana Wapalestina walishindwa kukivumilia, walipambana na polisi wa Kizayuni wakiwa mikono mitupu, na kupelekea Wapalestina 13 kati yao kuuawa shahidi. Masjidul Aqswa ni eneo takatifu kwa Waislamu wote, si kwa Wapalestina peke yao na ndio maana malalamiko ya Waislamu hadi leo hii yameenea kote ulimwenguni kuulaani utawala wa Kizayuni kwa kulikalia kwa mabavu eneo hilo tukufu.
Hasira zinazooneshwa na Wapalestina kutokana na vitendo vya kibeberu vya Israel katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas na dhidi ya vitendo vya kichokozi vinavyofanywa na Wazayuni katika Msikiti wa al Aqsa zinaonesha namna Wapalestina walivyo tayari kujitolea kwa mali na damu zao kulinda matukufu hayo ya Kiislamu.
Intifadha ya al Aqsa ilikuja baada ya Intifadha ya mawe iliyoanzishwa na wananchi wa Palestina mwaka 1987, na moja ya sifa za Intifadha ya al Aqsa, ni namna Intifadha hiyo iliyochukua sura ya kimataifa.
Intifadha hiyo iliuzuia utawala wa Kizayuni kufuatilia malengo yake haramu ya kujiimarisha katika ardhi za Wapalestina na kwa mara ya kwanza, Israel ililazimika kulegeza kamba na kulikimbia eneo la Ghaza mwaka 2005. Kwa hakika kukimbia Wazayuni katika Ukanda wa Ghaza ni miongoni mwa matunda muhimu sana ya Intifadha ya al Aqsa. Wananchi wa Palestina wamethibitisha kivitendo kwamba kamwe hawako tayari kuuruhusu utawala wa Kizayuni uishi salama katika ardhi za Palestina.
Kuanza Intifadha ya al Aqsa mwaka 2000 kulikokuja kwa lengo la kulalamikia jeuri ya viongozi wa utawala wa Kizayuni ya kuuvunjia heshima Msikiti wa al Aqsa, ni ushahidi wa wazi wa jambo hilo. Matukio mbalimbali ya Palestina nayo yamethibitisha kuwa, mapambano ya wananchi wa Palestina si tu hakuna siku yamewahi kusimama, bali kadiri siku zinavyopita ndivyo yanavyoingia katika awamu mpya na pana zaidi. Intifadha ya al Aqsa imekuja na matunda bora zaidi ikilinganishwa na Intifadha ya Mawe.
Intifadha hiyo ya al Aqsa imeandaa mazingira ya kuingia kwenye hatua ya mbele zaidi mapambano ya Wapalestina. Mara kwa mara Wapalestina wamekuwa wakisisitiza kuwa, Intifadha ya Tatu ni jambo lisiloepukika na tayari tumekuwa tukishuhudia utangulizi wa Intifadha hiyo. Amma cha kuvutia zaidi ni kwamba, sasa si katika Ukanda wa Ghaza tu, lakini hasa katika maeneo mengine ya Wapalestina hususan Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.