Hamas: Mapambano ya Intifadha ya Quds yataendelea
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imesisitiza kuendeleza mapambano ya Intifadha ya Wapalestina katika maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa Intifadha ya Quds.
Hamas imesisitiza katika taarifa yake juu ya kuendelezwa Intifadha na kueleza kuwa, harakati hiyo kwa mara nyingine tena inatangaza baiya na kufungamana kwake na wananchi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, huko Quds, Ukanda wa Ghaza na katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Hamas pia imetilia mkazo suala la kutetea haki zake na za wananchi wa Palestina mbele ya adui Mzayuni na kuuzuia utawala huo kutenda jinai dhidi ya Wapalestina.
Katika taarifa yake hiyo, Hamas kwa mara nyingine tena imetangaza kuwa haimtambui adui Mzayuni na kwamba haitasalimu amri kivyovyote vile mbele ya njama za Israel za kutaka kutwaa Quds na Masjidul Aqsa.
Taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas pia imelaani hatua ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuhudhuria mazishi ya mtenda jinai Shimon Perez na kuongeza kuwa, ushirikiano wowote na kuhuishwa uhusiano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na adui Mzayuni ni sawa na kuzisaliti damu za mashahidi wa Palestina na kuzichochea nchi za Magharibi zihuishe uhusiano wake na utawala ghasibu wa Israel.