Israel yawateka nyara wanaharakati wanawake wakielekea Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i16870-israel_yawateka_nyara_wanaharakati_wanawake_wakielekea_gaza
Jeshi la majini la utawala wa Kizayuni wa Israel limewateka nyara wanaharakati wanawake wa Marekani akiwemo Ann Wright, mwanadiplomasia mashuhuri na mtetezi wa haki za binadamu, wakiwa kwenye boti wakielekea katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 06, 2016 12:16 UTC
  • Israel yawateka nyara wanaharakati wanawake wakielekea Gaza

Jeshi la majini la utawala wa Kizayuni wa Israel limewateka nyara wanaharakati wanawake wa Marekani akiwemo Ann Wright, mwanadiplomasia mashuhuri na mtetezi wa haki za binadamu, wakiwa kwenye boti wakielekea katika Ukanda wa Gaza.

Ubalozi wa Marekani umethibitisha kuwa boti hiyo ya wanaharakati waliyokuwa wakielekea katika Ukanda wa Gaza, imetekwa na kuelekezwa kwa nguvu katika bandari ya utawala haramu wa Israel wa Ashdod.

Harakati ya CodePink inayosimamia msafara huo wa wanaharakati wa Kimarekani imetoa taarifa ikikosoa vikali hatua ya askari wa Israel kuiteka boti hiyo katika maji ya kimataifa. Taarifa ya harakati hiyo imesema boti hiyo haikuwa na silaha yoyote na kwamba nia ya wanaharakati hao ilikuwa kwenda kuvunja mzingiro wa Gaza pasina kutumia njia za mabavu.

Jeshi la utawala haramu likiteka nyara wanaharakati

 

Harakati ya CodePink imeitaka serikali ya Washington kuushinikiza utawala ghasibu wa Israel kuwaachia huru wanaharakati hao wa kike sambamba na kuanzishwa uchunguzi wa kutekwa boti hiyo isiyokuwa ya kivita katika maji ya kimataifa.

Mbali na Ann Wright, mwanadiplomasia na mwanaharakati mtajika wa Marekani, wengine waliokuwa kwenye boti hiyo ni Mairead Maguire, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, wabunge watatu na mwanariadha mashuhuri ambaye ni bingwa wa Olimpiki wa Marekani.

Israel inalizingira eneo la Ukanda wa Gaza kwa miaka kadhaa sasa ambapo raia zaidi ya milioni moja na nusu wa eneo hilo wanasumbuliwa na uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu kama chakula, maji na dawa.