Mivutano katika Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17635-mivutano_katika_baraza_la_mawaziri_la_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Hatua ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kung'ang'ania kuchukua mamlaka yote ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala huo, imepelekea kuibuka wimbi jipya la hitilafu na mivutano katika baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2016 23:41 UTC
  • Mivutano katika Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel

Hatua ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ya kung'ang'ania kuchukua mamlaka yote ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya utawala huo, imepelekea kuibuka wimbi jipya la hitilafu na mivutano katika baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu.

Duru za Kizayuni zinaarifu kuwa, baada ya Netanyahu kusisitiza kwamba, haoni haja ya kuweko maafisa katika Wizara ya Mashauri ya Kigeni, maafisa kadhaa katika wizara hiyo akiwemo Dore Gold, Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo wamejiuzulu, jambo ambalo limepelekea kuibuka ghadhabu na mivutano katika wizara hiyo.

Waziri Mkuu wa Israel ambaye kwa takribani miaka mitano alichukua mamlaka ya wizara hiyo kabla na

Benjamin Netanyahu na Waziri wa Nishati Yuval Steinitz

baada ya kujiuzulu Avigdor Lieberman nafasi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala huo, mwezi uliopita alifuta uamuzi wa kutumwa wawakilishi wa wizara hiyo nchini Marekani na Ulaya na kusisitiza kama ninavyomnukuu: "Hatuoni haja ya kuwa na maafisa wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni." 

Uamuzi huo wa Netanyahu uliwakasirisha mno maafisa wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Israel akiwemo mkurugenzi mkuu wa wizara hiyo Dore Gold. Aidha hatua hiyo ililalamikiwa na baadhi ya mawaziri. Katika matamshi yake baada ya hapo, Netanyahu alisema kuwa, sehemu ya majukumu ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni imekabidhiwa Wizara ya Ulinzi na kwamba, utekelezaji wa majukumu mengine umekabidhiwa pande nyingine za kisiasa nje ya wizara hiyo.

Baada ya matamshi hayo, Dore Gold Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni  ya Israel sambamba na kuelezea kutoridhishwa kwake na hali iliyojitokeza katika chombo cha kidiplomasia cha utawala huo alitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo.

Duru za Kizayuni zinaaamini kuwa, hatua ya Netanyahu ya kupuuza nafasi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni na kumtuma Waziri Tzachi Hanegbi nchini Marekani badala ya Dore Gold na kukubaliana na safari ya naibu wake yaani Michael Oren kwa ajili ya kwenda kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Ujerumani na Uholanzi ndiyo iliyoandaa mazingira ya kutokea hitilafu na mivutano baina ya viongozi wa utawala huo. 

Utendaji, matamshi na uamuzi wa Waziri Mkuu wa Israel pamoja na namna ya kuamiliana kwake na maafisa wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Israel unaonyesha kuwa, Netanyahu sambamba na kupuuza udiplomasia wa Israel anaamini kuwa, anafahamu masuala ya kisiasa na kidiplomasia kuliko hata wanadiplomasia wenyewe.

Kikao cha Baraza la Mawaziri la Israel

Pamoja na hayo, duru za Kizayuni zinaamini kuwa, kuongezwa mamlaka ya Netanyahu na kudhibiti uwezo wote wa chombo cha kidiplomasia cha utawala huo litakuwa kosa kubwa ambalo litakuwa na taathira hasi. Ron Ben-Yishai mchambuzi wa gazeti la Yediot Aharonot na Amir Bar Shalom mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Israel wanasema kuwa, hatua hizo zinaonyesha jinsi Netanyahu anavyoamini juu ya suala la kuongeza utumiaji mabavu, mivutano na mapigano.

Ukweli wa mambo ni kuwa, kuongezeka migawanyiko ya kisiasa ndani ya utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kushadidi migogoro ya utawala huo ikiwemo ya kiuchumi, kijamii na kimataifa ni mambo ambayo kivitendo yamepelekea kushtadi hali mbaya ya utawala huo ghasibu. 

Hapana shaka kuwa, hali hiyo ni kengele ya hatari kwa Baraza la Mawaziri la Netanyahu ambalo linahesabiwa kuwa moja ya mabaraza dhaifu na yaliyolegalega zaidi katika historia ya utawala huo haramu.