Viongozi wa Palestina wakutana Doha katika kikao nadra cha kutafuta umoja
Rais Mahmoud Abbas wa mamlaka ya ndani ya Palestina ameshiriki katika mkutano nadra na viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, mjini Doha, Qatar.
Siku ya Alhamisi, Abbas alikutana na mkuu wa idara ya kisiasa ya Hamas, Khaled Meshal na kiongozi wa harakati hiyo huko Ghaza, Ismail Haniya.
Duru zinadokeza kuwa mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, Saeb Eretak ambaye ni katibu wa Harakati ya Uombozi wa Palestina PLO na Balozi wa Palestina Qatar, Munir Ghanam.
Pande mbili zilijadili njia za kupunguza masaibu ya Wapalestina na pia kupunguza ufa uliopo baina ya Hamas na chama cha Fat'h cha Mahmoud Abbas.
Aidha viongozi wa Hamas walitoa wito wa kufanyika uchaguzi Palestina na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Hali kadhalika walipendekeza kuwepo harakati moja ya muungano wa Wapalestina ili kukabiliana na hujuma za utawala haramu wa Israel ambao pia unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Pande zote katika mkutano huo zimesisitiza umuhimu wa mazungumzo baina ya Fat'h na Hamas ili kufikia umoja wa kitaifa utakaofuatiwa na uchaguzi na serikali yenye kuwashirikisha Wapalestina wote.
Aidha pande zote ziliafiki kulinda 'Mradi wa Kitaifa wa Palestina' na kukabiliana na njama za Israel za kuvuruga kile walichokitaja kuwa ni suluhisho la 'mataifa mawili'.
Kwa muda mrefu sasa Wapalestina wamekuwa wakitoa wito kwa viongozi wao wanaohasimiana waungane na waelekeze nguvu zao katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.