Nov 05, 2016 03:36 UTC
  • Waandamanaji Bahrain
    Waandamanaji Bahrain

Wananchi wa Bahrain wameendelea kuandamana katika mji mkuu Manama na miji mingine ya nchi hiyo huku wakitangaza uungaji mkono wao kwa mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo Ayatullah Sheikh Isa Qassim na kutoa sha'ar za kuulaani utawala wa Aal Khalifa.

Mara baada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa na mtu mmoja mmoja hapo jana, waumini hao waliokuwa katika msikiti wa Imam Sadiq (as) uliopo katika eneo la al-Diraz mjini Manama walifanya maandamano na kulaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuzuia kusaliwa jamaa Sala ya Ijumaa pamoja na kuingia Imamu na waumini msikitini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo kwa muda wa wiki 15 sasa.

Tovuti ya Mir'at imeripoti kuwa waandamanaji hao walitoa sha'ar dhidi ya utawala wa Aal Khalifa na kutaka kupunguzwa ushawishi wa utawala huo, kukomeshwa dhulma za kimatapo, kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa na kusitishwa sera za kibaguzi zinazotekelezwa na utawala huo wa kiimla.

Wabahraini katika maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Isa Qassim

Wakati huohuo maelfu ya wananchi wa Bahrain jana walikusanyika mbele ya nyumba ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim na kutangaza uungaji mkono wao kwa mwanazuoni huyo.

Mwezi Juni mwaka huu utawala wa Bahrain ulimvua uraia Sheikh Isa Qassim, hatua ambayo imekabiliwa na upinzani mkali wa wananchi wa Bahrain na walimwengu kwa jumla.

Tangu mwezi Februari 2011, Bahrain imegeuka uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa Aal Khalifa.

Askari wa utawala wa Aal Khalifa wakiwakandamiza raia

Wananchi wa Bahrain wanataka yafanyike mageuzi ya kisiasa, kuwepo na uhuru na uadilifu, kuondolewe ubaguzi na vilevile ushike hatamu za uongozi wa nchi utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe; lakini utawala wa Aal Khalifa umekuwa muda wote ukijibu matakwa na madai halali na ya kisheria ya wananchi hao kwa kutumia mabavu na ukandamizaji.../

Tags