Amnesty yaitaka Uhispania iache kuiuzia Saudia meli za kivita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19306-amnesty_yaitaka_uhispania_iache_kuiuzia_saudia_meli_za_kivita
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Uhispania iache kuiuzia Saudi Arabia manowari za kijeshi na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ya Ulaya inapaswa kusitisha mauzo hayo kwa kuwa yumkini meli hizo za kivita zikatumika dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Nov 12, 2016 04:19 UTC
  • Amnesty yaitaka Uhispania iache kuiuzia Saudia meli za kivita

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Uhispania iache kuiuzia Saudi Arabia manowari za kijeshi na kusisitiza kuwa, nchi hiyo ya Ulaya inapaswa kusitisha mauzo hayo kwa kuwa yumkini meli hizo za kivita zikatumika dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.

Esteban Beltran, Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Uhispania amemtaka Mfalme Felipe VI kufuta makubaliano ya mauzo hayo huku akisisitiza kuwa, utawala wa Riyadh umekiuka sheria za kimataifa kutokana na jinai zake nchini Yemen na hivyo muamala kati ya nchi mbili hizo unapaswa kufutiliwa mbali.

Kadhalika Amnesty International imemtaka Mfamle Felipe VI wa Uhispania ambaye anatazamiwa kuitembelea Riyadh hii leo kutumia ushawishi wake kumtaka Mfalme Salman Bin Abdulaziz wa nchi hiyo asitishe mashambulizi ya anga ya miezi 20 ya utawala wa Aal-Saud dhidi ya watu wa Yemen.

Mfalme Felipe VI wa Uhispania

Uchunguzi wa hivi karibuni wa taasisi ya Stockholm International Peace Research Institute (SIPRI) ulibainisha kuwa, Saudi Arabia inashika nafasi ya kwanza kwa kununua silaha katika eneo la Mashariki ya Kati na kwamba uvamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudia nchini Yemen, umeifanya Saudi Arabia kuwa mnunuzi mkubwa wa silaha. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mwaka jana 2015, nchi hiyo ilinunua silaha zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 9 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Hujuma za Saudia nchini Yemen

Zaidi ya raia elfu 11 wa Yemen wameuawa tangu Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani na washirika weke wengine wa Kiarabu na Kimagharibi ilipoanzisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015.