Nov 13, 2016 16:41 UTC
  • Trump atahadharishwa na hatua ya kuuhamishia ubalozi wa Marekani Baitul Muqaddas

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amemtahadharisha rais mteule wa Marekani Donald Trump na kutekeleza ahadi aliyotoa ya kuuhamishia katika mji mtukufu wa Baitul Muqaddas ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv, Israel.

Riyadh Al-Mansour ametoa indhari hiyo kufuatia ahadi ambayo Trump aliitoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani kwamba atauhamishia katika mji mtakatifu wa Quds, Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.

Al- Mansour amesisitiza kuwa hatua hiyo ni ukiukaji azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na la Baraza Kuu la umoja huo na ni kufanya uadui wa dhahiri shahiri na taifa la Palestina.

Mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa ameashiria haki ya wananchi wa Palestina ya kutetea uwepo wao katika taasisi hiyo ya kimataifa na kusisitizia haki ya taifa la Palestina ya kuwa na uanachama wa kudumu katika Umoja wa Mataifa.

Trump (kushoto) na Netanyahu

Wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, Donald Trump ambaye wakati huo alikuwa mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais atauhamishia Baitul Muqaddas ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv.

Mwaka 1967, utawala ghasibu wa Israel ulivamia na kukalia kwa mabavu nusu ya mji mtukufu wa Baitul Muqaddas, na mnamo mwaka 1980 uliuunganisha mji huo na ardhi nyingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Mandhari ya Msikiti mtukufu wa al-Aqsa na Qubbat as-Sakhra katika mji wa Baitul Muqaddas

Marekani yenyewe pamoja na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa haiutambui uunganishaji huo kuwa ni halali kisheria kulingana na sheria za kimataifa na ndiyo maana kadhia ya Baitul Muqaddas ni suala la msingi linalopasa kujadiliwa na kutatuliwa katika mazungumzo ya amani na Wapalestina.../

Tags