Marufuku ya kuadhini katika misikiti ya Quds yaendelea kupingwa vikali
Naibu wa kwanza wa Spika wa Bunge la Palestina amesema kinyume na nia ya adui Mzayuni sauti ya adhana itasikika katika ardhi zote za Palestina.
Ahmad Bahr ameyasema hayo kupitia taarifa na kutangaza kuwa kupitishwa sheria ya kupiga marufuku kusomwa adhana katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na adui Mzayuni kumefanyika kwa lengo la kufanikisha njama ya kuuyahudisha mji huo na kufuta utambulisho wake wa Kiarabu na Kiislamu.
Amesema njama za utawala ghasibu wa Israel zitashindwa kutokana na kuendelea kusimama imara wananchi wa Palestina katika mji mtukufu wa Quds na ardhi zilizovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kusisitiza juu ya kuondoka wapinzani wa kusomwa adhana katika ardhi za Palestina kwa kuwa ni waqfu wa Kiislamu.
Naibu wa kwanza wa Spika wa Bunge la Palestina ametoa wito kwa Wapalestina wote wanaoishi katika mji wa Baitul Muqaddas na wanaolinda msikiti mtukufu wa Al-Aqsa kuendelea kukabiliana na siasa za kibaguzi za utawala wa Kizayuni na kutaka bunge la utawala huo haramu Knesset lifutiwe uanachama katika umoja wa mabunge duniani.
Wakati huohuo Ahmad al-Tib, mbunge wa bunge la utawala wa Kizayuni Knesset, siku ya Jumatatu alisoma adhana ndani ya bunge hilo kulalamikia marufuku ya kusomwa adhana katika misikiti ya mji wa Quds.
Siku ya Jumamosi ya tarehe 12 mwezi huu, Baraza la Mawaziri la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel lilipitisha sheria ya kupiga marufuku kusomwa adhana misikitini katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu za Baitul Muqaddas mashariki kwa madai kuwa inasababisha kero kwa baadhi ya wakaazi wa mji huo.../