Yemen yakaribisha vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1978-yemen_yakaribisha_vikwazo_vya_umoja_wa_ulaya_dhidi_ya_saudia
Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen amekaribisha kwa mikono miwili mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuiwekea vikwazo na marufuku ya kuuziwa silaha Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2016 04:43 UTC
  • Yemen yakaribisha vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Saudia

Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi nchini Yemen amekaribisha kwa mikono miwili mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuiwekea vikwazo na marufuku ya kuuziwa silaha Saudi Arabia.

Muhammad Ali al-Houthi amewaambia waandishi wa habari kwamba, mpango huu wa Umoja wa Ulaya unahesabiwa kuwa hatua muhimu ya umoja huo dhidi ya uvamizi wa Saudia na mashambulio yake ya kinyama dhidi ya raia wasio na hatia yanayofanyika kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Wananchi wa Yemen amesema kuwa, mpango huo wa Umoja wa Ulaya wa kuwekewa vikwazo Saudia na kupigwa marufuku kuuziwa silaha unaonesha jinsi umoja huo ulivyoelewa ukubwa wa maafa ya Yemen. Muhammad Ali al-Houthi ameashiria njama na ukwamishaji mambo wa Saudia na Marekani katika mwenendo wa kisiasa na mazungumzo ya ndani nchini Yemen na kubainisha kwamba, madola hayo yanafanya njama za kulitwisha matakwa yao taifa la Yemen. Jana Bunge la Ulaya lilipasisha azimio la kutaka Saudi Arabia iwekewe vikwazo vya silaha kutokana na vikosi vya jeshi la utawala wa Aal-Saud kushadidisha hujuma zake dhidi ya taifa la Yemen.

Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Yemen tarehe 26 mwezi Machi mwaka jana, lengo likiwa ni kuisambaratisha harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani Rais mtoro na aliyejiuzulu wa Yemen, Abdu-Rabuh Mansour Hadi.