Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen lakubali usimamishaji vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19861-baraza_kuu_la_kisiasa_la_yemen_lakubali_usimamishaji_vita
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amekaribisha juhudi za kusimamisha vita kwa ajili ya kukomesha uvamizi wa Saudi Arabia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 20, 2016 23:30 UTC
  • Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen lakubali usimamishaji vita

Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amekaribisha juhudi za kusimamisha vita kwa ajili ya kukomesha uvamizi wa Saudi Arabia nchini humo.

Saleh Ali al Sammad, Mkuu wa Baraza Kuu la kisiasa la Yemen alisema hayo jana (Jumapili) na kulishukuru jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi wa Yemen kwa kusimama kidete kuilinda nchi yao mbele ya uvamizi wa kila namna unaoongozwa na Saudi Arabia.

Vile vile ametilia mkazo suala la umoja na mshikamano katika safu za Wayemen na kuongeza  kiwango cha kuwa kwao tayari kukabiliana na njama zozote zile dhidi ya taifa lao.

Wasaudia wanatumia hata silaha zilizopigwa marufuku kushambulia wananchi wa Yemen

 

Sadiq al Sharafi, afisa wa kambi ya wananchi wa Yemen amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Mehr kwamba, Ismail Ould Cheikh Ahmed, mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen anafanya upendeleo katika suala hilo na kila inapotokezea Marekani kutangaza usimamishaji vita, mara zote huwa ni kwa lengo la kuwaokoa Wasaudia waliokwama kwenye kinamasi.

Vile vile amelaumu utendaji wa Umoja wa Mataifa katika suala la Yemen na kuongeza kuwa, hadi hivi sasa kumeshatangazwa usimamishaji vita mara kadhaa nchini Yemen lakini hakuna makubaliano hata mamoja yaliyoheshimiwa na Saudia na hadi leo hii Umoja wa Mataifa umeshindwa kuchukua hatua yoyote ile dhidi ya Wasaudia.

Usimamishaji vita wa masaa 48 ulianza kutekelezwa juzi Jumamosi nchini Yemen, lakini muda mchache baadaye Wasaudia walifanya mashambulizi kwenye miji kadhaa ya nchi hiyo na kuvunja usimamishaji vita huo.