Nov 27, 2016 05:41 UTC
  • Al Maliki: Uwahabi uwekwe kwenye orodha ya makundi ya kigaidi

Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq ametoa wito wa kuwekwa kundi la Kiwahabi katika orodha ya makundi ya kigaidi duniani.

Nuri al Maliki amesema kuwa, shambulizi la kigaidi lililolenga watu waliokuwa wanatoka kuzuru Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein katika mji wa Hilla nchini Iraq ni ugaidi dhidi ya Uislamu na njama ya kutaka kuzusha mapigano na hitilafu kati ya Waislamu zinazopangwa na kuongozwa na Uwahabi na kundi la Daesh.

Mwenyekiti wa Muungano wa Utawala wa Sheria nchini Iraq amesema kuwa, Waislamu wa madhehebu zote mbili za Shia na Suni wanaelewa vyema hatari ya mapigano na vita vya kimadhehebu na kwa sababu hiyo kuna ulazima wa jamii ya dunia kuutambua Uwahabi kuwa ni kundi la kigaidi.

Maiti za Waislamu waliouwa katika shambulizi la kigaidi la Hilla

Mlipuko wa bomu la kutegwa garini uliotokea Alkhamisi iliyopita katika eneo la Shomali kwenye mji wa Hilla nchini Iraq umeua shahidi Waislamu zaidi ya mia moja wa madhehebu ya Shia waliokuwa safarini baada ya kuzuru kaburi la mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Karbala na kujeruhi wengine wengi. Kundi la kigaidi la Daesh linalofadhiliwa na Saudi Arabia limejigamba kuwa, ndilo lililofanya mauaji hayo.  

Tags