Israel yakasirishwa na muendelezo wa vikwazo vya Ulaya dhidi yake
Baada ya Ufaransa kutoa maagizo mapya kwa ajili ya kubandika stika katika bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, hatua hiyo imekabiliwa na radiamali hasi na kuikasirisha Israel.
Ufaransa imetoa maagizo hayo ambayo yanataka kutekelezwa sheria za Umoja wa Ulaya za kuweka stika katika bidhaa zinazotengenezwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Baitul Muqaddas ya Mashariki. Hii ni katika hali ambayo jamii ya kimataifa inayatambua maeneo hayo kuwa ni ardhi zilizoghusubiwa za Wapalestina ambazo ziliporwa na Israel katika vita vya mwaka 1967. Maagizo hayo yaliyochapishwa kwenye tovuti ya serikali ya Ufaransa yanaeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, miinuko ya Golan huko Syria na Ukingo wa Magharibi unaojumuisha Baitul Muqaddas ya Mashariki, si sehemu ya Israel. Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Israel imetangaza katika radiamali yake kwa hatua hiyo kwamba, inasikitisha kuona kuwa Ufaransa ambayo ina sheria inayopinga vikwazo inatekeleza sheria ambayo inaweza kuchochea aina fulani ya harakati ya kuisusia Israel.
Uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kubandika stika katika bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika miaka ya hivi karibuni, umewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa utawala wa Kizayuni. Kamisheni ya Ulaya imesema kuwa ni lazima kuweka stika maalumu katika bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu licha ya utawala wa Kizayuni kupinga suala hilo. Uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya unajumuisha maagizo yaliyotolewa juu ya ulazima wa kubandikwa stika juu ya bidhaa zinazotengenezwa kwenye vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Baitul Muqaddas ya Mashariki na katika miinuko ya Golan; maeneo ambayo yote yalivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 6 mwaka 1967. Imeelezwa kuwa, taasisi za kiraia katika baadhi ya nchi za Ulaya katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikitekeleza uamuzi huo wa kubandika stika katika bidhaa zinazozalishwa kwenye vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa njia mbalimbali na ni dhahir shahir kuwa harakati hizo za wananchi ndizo zilizoasisi harakati ya kususia bidhaa za Israel na hivyo kutoa msukumo kwa serikali za Ulaya katika uwanja huo. Radiamali za kimataifa zinazotolewa kila uchao dhidi ya jinai na kupenda kujitanua kwa utawala wa Kizayuni kufuatia mashikinikizo ya fikra za waliowengi ulimwenguni zinadhihirisha kuwa, utawala huo unazidi kupoteza uungaji mkono wake kimataifa; huku jamii ya kimataifa ikionyesha chuki na hasira zake kwa utawala huo kwa njia mbalimbali. Hatua kama hizi zinadhihirisha namna utawala ghasibu wa Israel unavyozidi kutengwa zaidi na zaidi katika uga wa kimataifa.
Vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Israel kimataifa hadi sasa vimeusababishia utawala huo hasara nyingi za kiuchumi. Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti kuwa, kiwango cha hasara iliyopata Israel katika sekta ya uchumi mwaka uliopita kinafikia karibu dola bilioni tisa na nusu kutokana na vikwazo mtawalia vya Umoja wa Ulaya kwa utawala huo ghasibu.