Wapinzani nchini Kuwait washinda karibu nusu ya viti vya Bunge
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20287-wapinzani_nchini_kuwait_washinda_karibu_nusu_ya_viti_vya_bunge
Wapinzani nchini Kuwait wameshinda karibu nusu ya viti vya Bunge la nchi hiyo kufuatia matokeo yaliyotangazwa leo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 27, 2016 10:34 UTC
  • Wapinzani nchini Kuwait washinda karibu nusu ya viti vya Bunge

Wapinzani nchini Kuwait wameshinda karibu nusu ya viti vya Bunge la nchi hiyo kufuatia matokeo yaliyotangazwa leo.

Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kuwait kuna shakhsia maarufu wa Harakati ya Kiislamu ya Katiba yenye mfungamano na Ikhwanul Muslimiin wamefanikiwa kuingia katika Bunge la nchi hiyo.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, wapinzani wamejinyakulia viti 24 kati ya viti 50 vya Bunge la Kuwait.

Aidha wanasiasa sita wa Kishia wameibuka na ushindi katika uchaguzi huo wa Bunge akiwemo Khalid al-Shatti mtaalmu mashuhuri wa sheria na Saleh Ashour Mbunge mashuhuri wa Kishia wa nchi hiyo.

Saleh Ashour mmoja wa Wabunge wa Kishia nchini Kuwait

Ripoti zinaonyesha pia kuwa, Safaa al-Hashem ndiye mwanamke pekee kati ya wagombea 14 wanawake aliyeibuka na ushindi katika uchguzi huo wa Bunge la Kuwait.

Uchaguzi wa Bunge nchini Kuwait ulifanyika jana katika vituo vitano cha uchaguzi ikiwa ni uchaguzi wa mapema baada ya Bunge kuvunjwa. Mfalme wa Kuwait, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Sabah alitoa amri ya kuvunjwa bunge la kitaifa la nchi hiyo ili kuandaa mazingira ya uchaguzi wa kabla ya wakati ikiwa ni punde tu baada ya serikali kujiuzulu.

Serikali ya Kuwait  ilitangaza kujiuzulu kufuatia msuguano baina yake na bunge. Mgongano baina ya mihimili hiyo miwili ya dola  nchini Kuwait ulitokana na hatua ya serikali kuidhinisha nyongeza ya bei ya mafuta ya petroli jambo ambalo wabunge walipinga vikali.