Israel yalazimika kurudi nyuma, yaakhirisha tena kujadili marufuku ya adhana
Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel (Knesset) limelazimika kulegeza kamba na kuakhirisha kujadili muswada wa kupiga marufuku adhana katika misikiti ya mji mtakatifu wa Quds, ukiwemo Msikiti wa al Aqsa ambao ni Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Duru za habari za Palestina zimeripoti habari hiyo na kuwanukuu Ahmad Tibi na Masoud Ghanaim, wajumbe wawili wa Bunge la Israel wakisema kuwa, muswada wa kupiga marufuku adhana ilikuwa ujadiliwe tena jana (Jumatano) lakini umeakhirishwa hadi Jumatatu ijayo.
Ghanaim amesema, wabunge Waarabu katika bunge la Knesset wanaendelea kuupinga kwa nguvu zao zote muswada huo kwani lengo lake ni kuwapokonya Waislamu haki na uhuru wao wa kuabudu.
Ikumbukwe kuwa Jumapili ya tarehe 13 Novemba, Baraza la Mawaziri la serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel lilipasisha sheria ya kibaguzi ya kupiga marufuku kusomwa adhana katika misikiti ya mji mtakatifu wa Quds.
Makundi mbalimbali ya Palestina yamelaani vikali hatua hiyo ya kichokozi na kusema kuwa hivyo ni vita vya wazi vya kidini vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni kwa lengo la kuwatoa Wapalestina katika mkondo wao wa kupambana na utawala huo pandikizi.
Hatimaye mashinikizo ya wananchi na viongozi wa Palestina yanaonekana kuzaa matunda na bunge la Israel limeamua kuakhirisha zoezi la kuujadili muswada huo bungeni ili kutathmini hali ya mambo. Hii ni mara ya pili kwa bunge hilo kuakhirisha mjadala huo ambao uliakhirishwa kwa mara ya kwanza Jumanne ya wiki iliyopita, na jana Jumatano umeakhirishwa tena hadi wiki ijayo.