Haniya: Muqawama wa Palestina umejiweka tayari kukabiliana na utawala wa Israel
Naibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema vikosi vya wanamuqawama wa Palestina vimejiweka tayari kikamilifu kukabiliana na mashambulio yanayoweza kufanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
Ismail Haniya ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ameyasema hayo katika hotuba za Sala ya Ijumaa huko Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa wanamapambano wa Brigedi za al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas wanaendelea kujizatiti na kujiweka tayari kwa makabiliano yoyote na utawala wa Kizayuni.
Haniya ameongeza kuwa brigedi za al-Qassam pamoja na makundi mengine ya muqawama yanaendelea kujiweka tayari muda wote kuanzia angani na ardhini, baharini na chini ya ardhi kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Israel.
Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas aidha ametoa wito juu ya ulazima wa kuwepo umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina katika kukabiliana na ukaliaji wa mabavu na jinai za utawala wa Kizayuni.
Ismail Haniya amesisitiza pia kuhusu udharura na umuhimu wa umoja wa kitaifa baina ya Wapalestina wenyewe kwa ajili ya kukabiliana na utawala haramu wa Kizayuni.../