PLO yaionya Marekani kuhusu kuhamishia ubalozi Quds Tukufu
Afisa wa ngazi za juu katika Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO amemuonya rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu pendekezo lake la kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Qud Tukufu.
Saeb Erekat amesema hatua kama hiyo itapelekea kuangamia mpango wa kile kinachotajwa kuwa ni mazungumzo ya amani ya Palestina na Israel.
Erekat ambayo ni Katibu Mkuu wa PLO ametoa kauli hiyo Ijumaa siku moja baada ya Trump kutangaza kumteua mwanasiasa Myahudi mwenye misimamo mikali David Friedman kama balozi wa Marekani katika utawala bandia wa Israel.
Friedman anajulikana kwa uungaji mkono wake mkubwa kwa sera haramu za Israel za kujenga vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina.
Jana Ijumaa pia Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, Palestina inayokaliwa kwa mabavu amesema, kuhamishiwa Baitul Muqaddas ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv na kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel ni sawa na kutangaza vita na Wapalestina na Waislamu duniani kote.