Ja'fari akosoa njama zinazofanywa na nchi za Magharibi nchini Syria
Mwalikishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa amekosoa njama zinazofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa kwa ajili ya kuingilia mambo ya ndani ya Syria.
Bashar al Ja'fari amesema kuwa Marekani, Uingereza na Ufaransa zinafanya jitihada za kutaka kuwaonesha walimwengu kwamba, zimefanikiwa kupasisha azimio la kuundwa kikosi kipya cha kimataifa cha kusimamia hali ya kibinadamu katika ene la Aleppo nchini Syria, lakini mwenendo na juhudi hizo ni za uongo na za kinafiki.
Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, jumuiya mbalimbali za misaada ya kibinadamu kama Jumuiya ya Hilali Nyekundu, Shirika la Msalaba Mwekundu, Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa na asasi zisizo za serikali zinafanya kazi nchini Syria na kwamba Damascus inataka jumuiya hizo zepewe misaada na zana za kutosha kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kibinadamu.
Katika siku za hivi karibuni jeshi na makundi ya mapambano ya Syria yamefanikiwa kukomboa karibu maeneo yote yaliyokuwa yametekwa na makundi ya kigaidi. Mafanikio hayo yameyatia kiwewe makundi ya kigaidi na waungaji mkono wao kama Marekani, Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel.