Hizbullah: Tutabakia Syria hadi magaidi wote waangamizwe
Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah amesema wanamapambano wa muqawama wako nchini Syria katika fremu ya ushirikiano na serikali ya Damascus na kusisitiza kuwa wataendelea kubakia nchini humo hadi magaidi watakapotokomezwa kikamilifu.
As-Sayyid Ibrahim Amin As-Sayyid, ameyasema hayo baada ya mazungumzo na kiongozi wa Wakristo wa madhehebu ya Maroni Kadinali Bashara Putros Raí. Akizungumzia wito wa Uturuki wa kuzitaka pande zote za kigeni ikiwemo Hizbullah ziondoke nchini Syria, Mkuu wa Baraza la Kisiasa la harakati hiyo ya muqawama amesema, Hizbullah itaondoka nchini humo wakati wowote ule itakapoona ni mwafaka na kuna maslaha ya kufanya hivyo.
Ibrahim Amin As-Sayyid amebainisha kuwa ikiwa magaidi watapata ushindi nchini Syria watasababisha madhara kwa eneo zima; na kutokana na sababu za kijiografia na kihistoria, Lebanon itakuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kupatwa na madhara hayo.
Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Hizbullah ameashiria pia kukombolewa mji wa Halab kutoka kwenye makucha ya magaidi na kueleza kwamba kukombolewa mji wa Halab ni hatua muhimu katika harakati ya kuushinda mkakati wa kigaidi; na pande zote zinapaswa kuyatumia mafanikio hayo kwa ajili ya kuleta uthabiti zaidi katika eneo…/