Wanazuoni wa Bahrain walaani mzingiro katika kijiji cha Diraz
Wanazuoni nchini Bahrain wamekosoa vikali na kutoa wito wa kuondolewa mzingiro dhidi ya kijiji cha Diraz, anakoishi msomi na mwanaharakati wa Kiislamu nchini humo Sheikh Isa Qassim.
Kanali ya televisheni ya al-Manar imenukuu taarifa ya Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu nchini Bahrain iliyosema kuwa: "Lengo la utawala wa Aal-Khalifa kuweka mzingiro huo ni kujaribu kuwashinda na kuwaondoa wakazi wa kijiji hicho katika kufikia malengo na matakwa yao ya kisheria."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, utawala wa Manama umeweka vizuizi zaidi ya 20 katika njia za kuingia Diraz, sambamba na kuzuia maji safi na chakula kwa wakazi wa kijiji hicho.
Sheikh Hussein al-Daihi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani cha Waislamu wa Bahrain hapo jana aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Katika hali ambayo jamii ya kimataifa imekuwa ikilaani na hata kutoa mashinikizo ya kuvunjwa mizingiro ya kidhalimu katika maeneo mbali mbali ya dunia, lakini imeamua kufumbia macho kwa makusudi mzingiro katika eneo la Diraz." Alifafanua kuwa, mzingiro huo wa zaidi ya siku 200 umewaathiri wakazi zaidi ya 20,000, hii ikiwa ni adhabu ya muda mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya eneo hilo.
Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga kuvuliwa uraia Sheikh Isa Qassim kwa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti anachochea malumbano ya kimadhehebu na ghasia. Sheikh Qassim ni mashuhuri kwa misimamo yake ya kutetea Umoja wa Kiislamu na maandamano ya amani Bahrain.