Idadi ya wazayuni walioangamizwa katika shambulio la Quds yafikia sita
Duru za Palestina zimetangaza kuwa idadi ya wazayuni walioangamizwa katika operesheni ya shambulio iliyotekelezwa na kijana mmoja wa Kipalestina imefikia sita baada ya wazayuni wengine wawili waliojeruhiwa katika shambulio hilo kufariki dunia. Wazayuni wengine wasiopungua 20 walijeruhiwa katika shambulio hilo.
Fadi al Qanbar, ambaye ni miongoni mwa wafungwa walioachiliwa huru kutoka magereza ya utawala haramu wa Israel jana alitekeleza operesheni dhidi ya wazayuni kwa kuendesha lori lililowagonga na kuwaponda askari kadhaa wa Kizayuni waliokuwa wameteremka kwenye basi katika eneo la Armon HaNetziv, kusini mwa Baitul Muqaddas Mashariki.
Wakati huohuo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeeleza kwamba operesheni iliyotekelezwa jana dhidi ya askari wa Kizayuni imeonesha kuwa Intifadha ya Quds haikuwa tukio la kupita.
Msemaji wa Hamas Fawz Barhum amesisitiza kuwa njama zote zinazofanywa kila mara ili kuisaliti au kuizima Intifadha ya Quds zitagonga mwamba.
Naye Daud Shahab, msemaji wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina amesema kuhusiana na operesheni ya muqawama iliyotekelezwa na kijana wa Kipalestina kwamba hilo ni jibu la kutarajiwa kutolewa dhidi ya jinai ambazo utawala wa Kizayuni unawatendea wananchi wa Palestina…/