Sheikh Naim Qassim: Hizbullah itaendelea kubakia Syria kadiri itakavyohitajika kufanya hivyo
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo itaendelea kubakia nchini Syria na kupambana na magaidi wa kitakfiri kadiri itakavyohitajika kufanya hivyo.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la ad-Diyar la nchini Lebanon na kubainisha kwamba, kukabiliana na ugaidi wa kitakfiri ni sehemu isiyotenganishika na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amebainisha kwamba, ni vigumu kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuendesha vita vya moja kwa moja peke yake na ndio maana utawala huo ghasibu umekuwa ukishirikiana na serikali ya Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika Mashariki ya Kati kwa ajili ya kuendesha vita visivyo vya moja kwa moja.
Sheikh Naim Qassim amekosoa pia siasa za utawala wa Aal Saud katika Mashariki ya Kati na kubainisha kwamba, misimamo ya Hizbullah dhidi ya Saudi Arabia ina uhusiano na siasa hasi, makosa na uwendawazimu wa Saudia mkabala na mataifa ya eneo hili.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema bayana kwamba, Saudia inapaswa kuachana na mwenendo wake usio sahihi na badala yake ishughulike kuyatafutia ufumbuzi matatizo na migogoro ya Mashariki ya Kati kupitia njia ya kufahamiana na madola makubwa na yenye taathira katika eneo hili.