Arab League, Iraq zalaani ubaguzi wa Trump dhidi ya Waislamu
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeeleza wasi wasi wake mkubwa juu ya hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kupasisha sheria ya kuwazuia wakimbizi na raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia Marekani.
Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League amesema uamuzi huo wa Trump hauwezi kuhalalishika kwa njia yeyote ile na ni hatua ya kibaguzi.
Jumuiya hiyo ambayo ina nchi wanachama 22 imemtaka Trump kuangalia upya sheria hiyo, ambayo inasema kutekelezwa kwake kutakua na taathira hasi sio tu kwa Marekani, bali pia kwa umoja wa familia za nchi zilizoathiriwa, sambamba na kuandaa mazingira ya kuvunjika mazungumzo kati ya jamii ya Waarabu na Wamarekani.
Wakati huo huo, mwanachuoni maarufu wa Kishia nchini Iraq, Sayyid Muqtada al-Sadr, amelaani sheria hiyo ya kibaguzi ya Trump, akisema kuwa wakati umefika wa serikali ya Baghdad nayo iwatimue nchini Iraq Wamarekani.
Msomi huyo wa Kiislamu amesema kuwa: "Itakuwa ni upumbavu wa hali ya juu kuwaruhusu Wamarekani waingie na kutoka Iraq na nchi zingine zilizopigwa marufuku watakavyo, ilhali raia wa nchi hizo wamewekewa vizuizi vya kuingia Marekani.
Huku hayo yakiarifiwa, Kamati ya Masuala ya Nje ya Bunge la Iraq imekosoa vikali uamuzi huo wa serikali ya Washington na kufafanua kuwa, Iraq imekuwa katika mstari wa mbele wa kupambana na ugaidi, na sio haki kuwabagua Wairaqi kwa kiwango hiki."
Ijumaa iliyopita, Trump ilipasisha sheria ya kutoruhusiwa nchini Marekani kwa muda wa miezi mitatu wakimbizi na watu kutoka nchi zenye idadi kubwa ya Waislamu, ambazo ni Iran, Iraq, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.