Kuwait yakanusha madai ya kupiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i24747-kuwait_yakanusha_madai_ya_kupiga_marufuku_raia_wa_nchi_za_kiislamu
Serikali ya Kuwait imekadhibisha habari ya tetesi iliyoenea katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba nchi hiyo imepiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 05, 2017 23:12 UTC
  • Kuwait yakanusha madai ya kupiga marufuku raia wa nchi za Kiislamu

Serikali ya Kuwait imekadhibisha habari ya tetesi iliyoenea katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba nchi hiyo imepiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia nchini humo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait imesema serikali ya nchi hiyo haijatoa agizo hilo la kuwazuia raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia nchini humo. Wizara hiyo imesema kuwa, nchi zinazodaiwa kuwa zimepigwa marufuku kuingia nchini humo zina uhusiano mzuri na wa kipekee na nchi hiyo na raia wao wanaingia Kuwait kila leo.

Aghalabu ya vyombo vya habari vya Magharibi vilichangamkia uvumi huo, huku Rais wa Marekani Donald Trump akipongeza tetesi hizo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook. 

Bendera ya Kuwait

Taarifa hiyo ya tetesi ilidai kuwa, Kuwait imewapiga marufuku raia wa nchi za Syria, Iraq, Iran, Pakistan na Afghananistan kuingia nchini humo, siku chache baada ya Marekani kutoa amri kama hiyo.

Hivi karibuni, Trump alipasisha amri tata ya kuwazuia raia wa Iran, Iraq, Syria, Yemen, Sudan, Libya na Somalia kuingia nchini humo. Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ya Marekani imekataa ombi la Ikulu ya Rais wa nchi hiyo la kudumishwa marufuku ya kuingia raia wa nchi za Kiislamu nchini Marekani.

Hukumu ya kusimamisha amri ya Rais Donald Trump wa Marekani inayowazuia raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia Marekani ilitolewa Ijumaa na Jaji James Robart.

Rais Donald Trump wa Marekani