Zuma: Afrika Kusini itaendelea kuwaunga mkono watu wa Palestina
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amezihimiza nchi zote duniani ziendelee kuwaunga mkono na kuwatetea watu wanaokandamizwa wa Palestina.
Zuma ambaye jana alikuwa akihutubia Bunge la Afrika Kusini amekemea ukiukaji wa sheria na maazimio ya kimataifa unaofanywa na Israel na kusisitiza kuwa, Pretoria itaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina katika mapambano yake ya ukombozi na dhidi ya siasa za ukandamziaji za utawala huo.
Rais wa Afrika Kusini amesema, mwaka 2017 ni mwaka wa 50 tangu ardhi ya Palestina ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kuongeza kuwa, sera na siasa za Israel za kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina zinavuruga jitihada za kimataifa zinazolenga kuundwa nchi huru ya Palestina.
Mwezi uliopita pia Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini wakati wa sherehe za kutimia mwaka wa 105 tangu chama tawala cha ANC kilipoasisiwa, aliwataka wananchi wa nchi hiyo kuonesha mshikamano na watu wanaokandamizwa wa Palestina kwa kutofanya safari katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi.