Kongamano la mabunge ya Kiarabu na mustakbali wa Palestina
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu ameelezea kuwepo migongano ya serikali mpya ya Marekani kuhusu masuala ya ulimwengu wa Kiarabu.
Katika ufunguzi wa kongamano la mabunge ya Kiarabu lililofanyika jana Jumamosi huko mjini Cairo, Misri, Ahmed Aboul Gheit alielezea kuwepo matamshi yenye ishara za kugongana katika serikali mpya ya Marekani na kuongeza kuwa: "Tunafadhilisha kuendelea kusubiria matukio ya baadaye." Mwisho wa kunukuu. Ameongeza kuwa, hadi sasa ni mapema sana kuhukumu juu ya misimamo yote ya serikali mpya ya Marekani kuhusiana na ulimwengu wa Kiarabu.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu ameongeza kuwa, bado kuna baadhi ya misimamo ya kutia wasi wasi juu ya mustakbali wa taifa la Palestina. Kongamano la Mabunge ya Kiarabu lilianza Jumamosi ambapo washiriki walijadili matukio ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati na hujuma za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Palestina, nafasi ya mabunge na asasi za Kiarabu katika kuunga mkono msimamo wa Palestina kwa ajili ya kurejesha haki zake zilizoghusubiwa na kadhalika kuundwa serikali huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu.
Imepangwa kwamba washiriki wa kongamano hilo watatoa ripoti ambayo itawasilishwa katika kongamano la 28 la viongozi wa nchi za Kiarabu litakalofanyika mwezi Machi mwaka huu huko nchini Jordan. Inaelezwa kuwa, siasa za kupingana na kadhalika misimamo ya kushangaza ya Rais Donald Trump wa Marekani, ndiyo imewafanya viongozi wa nchi za Kiarabu kupatwa na wasi wasi kuhusiana na Washington. Katika mazingira hayo, nchi tofauti sambamba na kukosoa siasa za ndani na nje za Marekani zimezitaja kuwa ni aina fulani ya kutozingatia mahusiano na mataifa mengine. Ni suala lisilo na shaka kwamba misimamo ya Washington katika masuala ya Palestina, bado haijawa wazi. Hii ni katika hali ambayo katika kampeni za uchaguzi na hata baada ya kushinda kwake uchaguzi huo, Donald Trump ametoa matamshi ya kuunga mkono ujenzi wa vitongozi vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapelstina.
Kadhalika rais huyo aliunga mkono mpango wa kuhamishwa ubalozi wa Marekani ulioko Tel-Aviv na kupelekwa Baitul-Muqaddas, suala ambalo limekosolewa vikali na pande mbalimbali duniani. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni na kutokana na mashinikizo ya fikra za walio wengi, rais huyo wa Marekani ameamua kulegeza misimamo yake hiyo mikali kuhusu masuala mengi ya kimataifa. Pamoja na hayo siasa zisizofahamika za rais huyo hususan kuhusu matukio ya Mashariki ya Kati zimeendelea kuibua wasi wasi katika ngazi tofauti za kimataifa. Kuhusu suala hilo, misimamo ya kindumakuwili ya madola ya Kiarabu nayo imeendelea kukosolewa na fikra za walio wengi.
Hii ni kusema kuwa, siasa za kijuba za baadhi ya nchi za Kiarabu katika kushirikiana na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, si tu kwamba zimesababisha kutotatuliwa migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati hususan nchini Syria na Iraq, bali zimelifanya suala la utatuzi wa mgogoro wa Palestina, ambayo ndio kadhia kuu ya ulimwengu wa Kiislamu kufeli. Ni suala lililo wazi kwamba madamu nchi za Kiarabu na asasi zenye mafungamano na nchi hizo zitaendelea kufuata maamuzi ya Marekani, kamwe hazitaweza kuwa na nafasi chanya katika utatuzi wa matukio ya kieneo na kimataifa. Hii ni kusema kuwa, baadhi ya viongozi wa Kiarabu badala ya kufuatialia masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu hususan mustakbali wa taifa la Palestina, ndio kwanza zimeendelea kuchochea moto wa ugaidi na migogoro ya mauaji nchini Iraq, Syria na Yemen.