Russia yatilia mkazo kusimamishwa ujenzi wa vitongoji wa utawala wa Kizayuni
Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametaka kusimamishwa ujenzi iwa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.
Vitaly Churkin amesema kuwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ni kinyume na sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa. Churkin amebainisha kuwa jamii ya kimataifa inasisitiza kusimamishwa ujenzi wa vitongoji hivyo unaofanywa na Israel katika ardhi za Palestina ulizozighusubu. Knesset yaani bunge la utawala wa Kizayuni wiki iliyopita lilipasisha sheria ambayo kwa mujibu wake itahalalisha kuunganishwa ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kujengwa nyumba za walowezi wa Kiyahudi karibu elfu nne pia katika ardhi za Wapalestina itakuwa halali kisheria. Bunge la Israel limepasisha sheria hiyo ya kuziunganisha ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 23 mwezi Disemba mwaka jana lilipitisha azimio nambari 2334 ambalo lililaani na kutaka kusimamishwa ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.