Israel yaamua kuuteka kikamilifu Ukingo wa Magharibi
Waziri wa Mazingira wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema, baada ya kutokea mabadiliko katika utawala wa Marekani na kuingia madarakani Donald Trump, wakati umefika wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuuteka kikamilifu Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuuweka chini ya udhibiti wa Israel.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina kimemnukuu Zeév Elkin ambaye ni mbunge mwenye misiamo mikali ya Kizayuni akisema katika bunge la Israel kwamba, kupokonywa Wapalestina eneo lote la Ukingo wa Magharibi na kuwekwa chini ya udhibiti wa Israel ni jambo muhimu sana na inabidi hatua za kufanikisha jambo hilo zianze kuchukuliwa haraka katika kipindi hiki cha urais wa Donald Trump nchini Marekani.
Amma kuhusiana na Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Elkin amesema, mamlaka hiyo haina umri mrefu tena kwani baada ya urais wa Mahmoud Abbas, Mamlaka ya Ndani ya Palestina haitabakia tena, bali itaingia kwenye mkondo wa kuporomoka kikamilifu.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unachukua hatua za kikatili na za uporaji wa ardhi za Wapalsetina katika hali ambayo kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa, Israel imepigwa marufuku kujihusisha kivyovyote vile na ardhi za Wapalestina.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia mbinu na hila za kila namna za kilaghai ili kuficha ubeberu wake na kuandaa mazingira ya kuimarisha siasa zake za dhulma dhidi ya taifa madhlumu la Palestina.