Ismail Hania: Vita vya Palestina na Israel ni kuhusu Masjidul Aqswa
Naibu wa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, vita vya Palestina na utawala wa Kizayuni vinahusiana na Msikiti wa al Aqsa na utambulisho wa Palestina.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ismail Hania akisema hayo jana usiku katika sherehe za kufungua Msikiti wa Mashahidi wa Ridhwan mjini Ghaza na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel una nia ya kuvunja utambulisho wa umma wa Kiislamu na muqawama wa taifa la Palestina na ndio maana umezusha mpango wa kugawa matumizi ya Msikiti wa al Aqsa kwa mujibu wa mahali na wakati baina ya Waislamu na Wazayuni.
Kwa upande wake, Ahmad Bahar, Makamu wa Kwanza wa Spika wa Bunge la Palestina ameyataka makundi yote ya Palestina kuwa kitu kimoja katika kukabiliana na siasa za Rais Donald Trump wa Marekani zilizo dhidi ya Waarabu na Waislamu.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeongeza vitendo vyake vya kikatili na ubaguzi wa kizazi tangu alipoingia madarakani Donald Trump nchini Marekani. Walimwengu hasa Waislamu na Waarabu wamekasirishwa mno na siasa za kibaguzi za rais huyo wa Marekani.
Kituo cha Kizayuni kinachojulikana kwa jina la B'Tselem, Jumanne iliyopita kilitoa ripoti na kutangaza kuwa, mwaka 2016 idadi ya nyumba za Wapalestina zilizovunjwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Baytul Muqaddas zilifikia 782; na kiwango hicho hakijawahi kutokea katika miaka yote ya huko nyuma.