Ramadan Shalah: Utawala wa Kizayuni unakabiliwa na matatizo mengi
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islamu ya Palestina amesema kuwa, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel haupo katika hali nzuri na unakabiliwa na matatizo chungu nzima.
Ramadhan Abdullah Shalah ameyasema hayo leo katika kongamano la sita la kuunga mkono Intifadha ya Palestina linalofanyika mjini Tehran ambapo sanjari na kuashiria hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahiil-Udhma Sayyid Ali Khamenei kuhusiana na Palestina amesema kuwa, hotuba hiyo ni ujumbe muhimu kwa raia wa Palestina.
Amesisitiza kwa kusema kuwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni sisitizo la kuwataka Wapalestina waendeleze mapambano yao ya muda mrefu dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Ramadhan Abdullah Shalah amepongeza juhudi za thamani za viongozi wa serikali, bunge na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuandaa kongamano la kuunga mkono Intifadha ya Palestina na kusema kuwa, harakati hizo zinabainisha msimamo chanya na uthabiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono na himaya yake kwa raia madhlumu wa Palestina. Kadhalika Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islamu ya Palestina amefafanua kuwa, kinyume na madai yanayotolewa na Israel, utawala huo hivi sasa hauko katika hali nzuri.
Amesema kuwa hivi sasa Israel si tu kwamba haina hali nzuri, bali inakabiliwa na matatizo chungu nzima muhimu zaidi ikiwa ni kudhoofika kwa kasi nguvu zake. Kongamano la sita la kimataifa la kuunga mkono Intifadha ya Palestina lilianza Jumanne ya jana mjini Tehran chini ya uongozi wa Ali Larijani, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ( bunge.)