Hamas: Amani itapatikana Mashariki ya Kati kwa kuangamizwa Israel
(last modified Sat, 25 Feb 2017 02:39:19 GMT )
Feb 25, 2017 02:39 UTC
  • Hamas: Amani itapatikana Mashariki ya Kati kwa kuangamizwa Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, sharti la kuweko amani na uthabiti katika Mashariki ya Kati ni kuangamizwa utawala haramu wa Israel.

Hayo yamesemwa na Ali Baraka mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nchini Lebanon ambaye amesisitiza kuwa, ili amani na uthabiti viweze kupatikana katika eneo hili la Mashariki ya Kati basi kuna haja ya kuangamizwa utawala haramu wa Israel.

Ali Baraka amebainisha kuwa, kuungwa mkono Intifadha ya Palestina ni jambo lenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha amani na uthabiti wa eneo hili la Mashariki ya Kati.

Mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nchini Lebanon ameongeza kuwa, hii leo Palestina inahitajia mno himaya na uungaji mkono wa Umma wa Kiislamu, Kiarabu na watu huru duniani na kwamba, mkutano wa sita wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina uliomalizika Jumatano iliyopita hapa mjini Tehran ni uzingatiaji wa suala hilo.

Ali Baraka mwakilishi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nchini Lebanon

Amesema kuwa, mkutano huo ulikuwa na mafanikio hasa kutokana na kufanyika katika kipindi ambacho adui Mzayuni na serikali ya Marekani iliyo dhidi ya taifa la Palestina wanaendelea na njama zao huku Baraza la Mawaziri la Israel likiendelea na ujezni wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina. 

Aidha Ali Baraka amesema kuwa, kuna haja ya kuwekwa kando hitilafu na mivutano katika Mashariki ya Kati na kudumishwa umoja na mshikamno wa ndani na nje ya Palestina kwa ajili ya kukabiliana na adui Mzayuni.