Israel yaidhinisha sheria ya kupiga marufuku Adhana
Bunge la Utawala wa Kizayuni wa Israel, Knesset, limepitisha rasimu ya sheria ya kupiga marufuku adhana katika misikiti yote iliyopo katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu.
Taarifa zinasema, kwa mujibu wa vipengee vya rasimu hiyo ambayo ilipasishwa Jumatano katika Bunge la utawala wa Kizayuni, Adhana kwa vipaza sauti ni marufuku Quds Tukufu kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, adhana katika masaa mengine ya siku inapaswa kuwa kwa sauti ya chini sana ambayo imeainishwa; na msikiti utakaokiuka sheria hiyo utatozwa faini ya dola 1,200 za Kimarekani. Upigwaji marufuku huo wa adhana ulipendekezwa katika baraza la mawaziri la serikali ya mrengo wa kulia yenye misimamo mikali ya utawala wa Kizayuni.

Hii ni katika hali ambayo, Ahmad Ar Rawidhi Mjumbe wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) huko Palestina hivi karibuni alionya kuhusu utendaji wa serikali yenye misimamo mikali ya Israel katika Quds tukufu na kusema hatua hiyo ni mwanzo wa njama mpya za Wazayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa.
Kwa muda mrefu sasa utawala wa Kizayuni wa Israel na walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakitekeleza njama ya kufuta utambulisho wa Kiislamu na Ukristo katika Quds tukufu na badala yake kulipa eneo hilo utambulisho bandia wa Kizayuni.