Misri yasisitiza udharura wa kurejea Syria katika Arab League
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa, mgogoro wa Syria unakaribia kupata ufumbuzi wa kisiasa na kusisitiza kuwa upo udharura wa kurejea nchi hiyo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).
Akizungumza kwenye mahojiano na gazeti la al Watan, Sameh Shoukry amesisitiza kuwa mgogoro wa Syria unakaribia kupata ufumbuzi wa kisiasa na kwamba mpango wa kuirejesha Syria katika Arab League pia unapasa kujadiliwa na kutekelezwa iwe ni kwa kuchelewa au haraka.
Sameh Shoukr ameashiria ombi lililowasilishwa hivi karibuni na Ibrahim Jaafari, waziri mwenzake wa Iraq kwa ajili ya kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kueleza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq alizungumzia suala hilo katika kikao cha siku kadhaa zilizopita cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa jumuiya hiyo. Shoukry amesema kuwa Arab League inashughulilkia mambo ya Waarabu wote na kwamba hitilafu za kimitazamo zilizopo kati ya wanachama wake pia zinapasa kuhitimishwa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ameongeza kuwa, Syria ni nchi ya Kiarabu na inahesabiwa kuwa nguzo muhimu katika ngao ya Waarabu.
Akijibu swali kuhusu uwezekano wa nchi za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi kuendelea kupinga suala la kubakia madarakani Rais Bashar al Assad wa Syria, Sameh Shoukry ameeleza kuwa, nchi zote hivi sasa zimeweka kando wazo la kutaka kutumia njia ya kijeshi dhidi ya Syria na kwamba nchi hizo zinashiriki katika kuandaa mustakbali wa kisiasa wa Syria unaoungwa mkono na wananchi na serikali.