Wapalestina waandamana kupinga marufuku ya adhana Quds tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26268-wapalestina_waandamana_kupinga_marufuku_ya_adhana_quds_tukufu
Maelfu ya wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu wamefanya maandamano kulaani sheria iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge la Israel ya kupiga marufuku adhana katika mji mtakatifu wa Quds.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2017 03:52 UTC
  • Wapalestina waandamana kupinga marufuku ya adhana Quds tukufu

Maelfu ya wananchi wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu wamefanya maandamano kulaani sheria iliyopasishwa hivi karibuni na Bunge la Israel ya kupiga marufuku adhana katika mji mtakatifu wa Quds.

Takriban Wapalestina elfu 3 walishiriki maandamano hayo ya jana Jumamosi katika mji wa Kabul, ambapo walisikika wakipiga nara dhidi ya Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.

Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zisemazo: "Msinyamazishe adhana"...."Sheria dhidi ya adhana haitapita"....na "Tutazidisha sauti za adhana kila kona". 

Wapalestina wameweka vipaza sauti vya adhana katika paa za nyumba zao huku wakisisitiza kuwa, sauti ya adhana kamwe haitazimwa katika mji wa Quds.

Wapalestina wapinga marufuku ya adhana

Farhan Haq, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani hatua hiyo ya utawala bandia wa Kizayuni kupiga marufuku adhana na kusema Israel inapaswa kuheshimu haki za kidini za Wapalestina.

Ijumaa iliyopita, Islamail Haniya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, alisema kuwa: "Liwe liwalo, taifa la Palestina na Waislamu wataendelea kusoma adhana kote duniani."

Jumatano iliyopita, Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel (Knesset) lilipasisha hatua ya kwanza ya muswada wa sheria inayopiga marufuku adhana kwa vipaza sauti katika misikiti ya mji mtakatifu wa Quds kwa kura 55 za ndio na 48 za hapana, sheria itakayotekelezwa kuanzia saa tano usiku hadi saa moja asubuhi iwapo muswada huo utapita.