HAMAS kuendeleza juhudi za kuleta umoja baina ya Wapalestina
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema harakati hiyo itaendelea kufanya juhudi ili ufikiwe umoja na kukombolewa ardhi zote za Palestina.
Khalid Mash'al ameyasema hayo jana Jumatatu mjini Khartoum, Sudan katika majlisi ya kumuenzi na kumkumbuka Dakta Hassan Abdullah Turabi, mwanafikra mkubwa wa Kiislamu na kiongozi wa chama cha Kongresi ya Wananchi ya Sudan na kusisitiza kwamba Hamas itaendelea na juhudi zake za kufanikisha mkakati wa kufikiwa umoja pamoja na ukombozi wa Palestina.
Mash'al aidha ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Sudan kutokana na kifo cha Dakta Turabi.
Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya HAMAS ameeleza kuwa Dakta Turabi alikuwa mtetezi na muungaji mkono wa wananchi na malengo matukufu ya Palestina na daima alikuwa akifanya juhudi za kupatikana umoja baina ya Wapalestina.
Ujumbe wa viongozi wa Hamas ukiongozwa na Mash'al na kumjumuisha pia Musa Abu Marzouq, Maher Ubaid na Usama Hamdan uliwasili mjini Khartoum Jumapili usiku kwa madhumuni ya kwenda kutoa mkono wa pole kutokana na kifo cha Dakta Hassan Turabi.
Turabi, aliyekuwa na umri wa miaka 84, alifariki Jumamosi usiku kutokana na shinikizo la moyo.../