Spika wa Bunge Kuwait: Israel inapaswa kutengwa kimataifa
Spika wa Bunge la Kuwait, Marzouq Al-Ghanim, amelaani siasa za kibaguzi za utawala haramu wa Israel na kusisitiza udharura wa kutengwa utawala huo katika Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge.
Al-Ghanim ameyasema hayo katika mazungumzo yake na waandishi wa habari na kuongeza kuwa, msimamo wa Kuwait kuhusu Israel upo wazi na msimamo huo ndio unaotekelezwa katika siasa za kigeni za nchi hiyo.
Sambamba na kuashiria kwamba Israel haiheshimu sheria za kimataifa na kwamba inaendeleza siasa za uhasama dhidi ya Wapalestina, Spika wa Bunge la Kuwait amesema kuwa, licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio nambari 2234 linaloutaja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina kuwa sio sahihi, Bunge la Israel (Knesset) limeendelea kupuuza azimio hilo kwa kubariki uamuzi wa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel, wa kuendelezwa na ujenzi huo. Spika wa Bunge la Kuwait, amefafanua kuwa, mabunge ya nchi za Kiarabu yanatakiwa kuchukua hatua za kukabiliana na mienendo hiyo ya Israel kupitia mawasiliano na mabunge ya nchi nyingine ili kuzuia siasa za kujitanua za Tel Aviv.
Marzouq Al-Ghanim amesema kuwa, hivi sasa Kuwait imeanzisha majadiliano yenye lengo la kulitenga Bunge la Israel kimataifa kutokana na uvunjaji wake wa sheria za kimataifa na kwamba mabunge ya nchi za Kiarabu na Kiislamu yanatakiwa kufuata mkondo huo.
Hii ni katika hali ambayo, kwa mara kadhaa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sambamba na kutoa mwito wa kutaka kutengwa utawala huo ghasibu, imekuwa ikisisitiza pia juu ya kusambaratishwa kwake kutoka eneo la Mashariki ya Kati, suala ambalo limekuwa likikabiliwa na vikwazo kutokana na baadhi ya tawala za Kiarabu, hususan Saudi Arabia kujipendekeza kwa Israel na mabwana zake na kula njama dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Itafahamika kuwa, tarehe 23 Disemba mwaka jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipitisha azimio nambari 2234 linalolaani ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni unaofanywa katika ardhi za Wapalestina, azimio ambalo lilipigiwa kura ya ndio na wajumbe 14.