Onyo la taasisi za kimataifa kuhusu hali mbaya ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26948-onyo_la_taasisi_za_kimataifa_kuhusu_hali_mbaya_ya_yemen
Vita vya kivamizi vilivyoanzishwa na Saudi Arabia nchini Yemen vimeingia kwenye mwaka wake wa tatu katika hali ambayo vimeshasababisha maafa makubwa mno ya kibinadamu kiasi kwamba vimeanza kuzifanya taasisi za kimataifa zishindwe kuvumilia tena.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 27, 2017 23:25 UTC

Vita vya kivamizi vilivyoanzishwa na Saudi Arabia nchini Yemen vimeingia kwenye mwaka wake wa tatu katika hali ambayo vimeshasababisha maafa makubwa mno ya kibinadamu kiasi kwamba vimeanza kuzifanya taasisi za kimataifa zishindwe kuvumilia tena.

Moja ya mashirika ya kimataifa yaliyoonesha kusikitishwa mno na jinai zinazoendelea kufanywa na Saudia huko Yemen ni lile la Oxfam ambalo limetoa onyo kuhusu hali mbaya ya kibinadamu kwa wananchi wa Yemen kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na muungano wa nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia. Oxfam ambalo ni moja ya mashirika makubwa ya kimataifa yanayojishughulisha na kutoa misaada ya kibinadamu na kukomesha umaskini, njaa na ukosefu wa uadilifu duniani, linaundwa na taasisi 30 za misaada na mambo ya kheri za kimataifa. Katika ripoti yake hiyo, Oxfam limekumbusha kuwa, vita vya Yemen vilivyoanza zaidi ya miezi 24 iliyopita, vimeshapelekea kuuawa maelfu ya watu wasio na hatia.

Shirika hilo la kimataifa limesisitiza kuwa, kundi la nchi zinazoongozwa na Saudi Arabia kila siku linashambulia bandari, barabara, madaraja, maghala, mashamba, na masoko na hivyo kusababisha karibu watu milioni 17 wa Yemen ambao ni sawa na asilimia 60 ya wananchi wote wa nchi hiyo ya Kiarabu, wakabiliwe na janga la ukame na njaa.

Raia wa kawaida ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya kivamizi ya Saudia nchini Yemen

Saudia ilianzisha mashambulizi ya kivamizi mwezi Machi 2015 dhidi ya nchi maskini zaidi ya Kiarabu ya Yemen, kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, Israel na baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu na hivi sasa inaizingira nchi hiyo kutokea baharini, nchi kavu na angani kwa madai ya kutaka kumrudisha madarakani Abdu Rabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudia.

Maelfu ya wananchi wa Yemen wameshauawa na kujeruhiwa na mamilioni ya wengine wamekuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi hayo ya Saudia. Asilimia 80 ya miundombinu ya miji ya Yemen imeharibiwa kikamilifu. Yemen ina watu milioni 24, na hivi sasa milioni 21 kati yao wanahitajia misaada ya kibinadamu. Zaidi ya wananchi milioni 14 wa Yemen hawana usalama wa chakula. Hali ya watoto wadogo nchini humo ndiyo mbaya zaidi. Kwa mujibu wa mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, watoto milioni nane wa Yemen wanaishi katika ukata wa kupindukia kiasi kwamba katika kila watoto 10 wanane kati yao wanasumbuliwa na lishe duni.

Kuendelea kung'ang'ania viongozi wa Saudi Arabia kufanya mashambulizi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu ambayo hata kabla ya kuvamiwa ilikuwa na idadi kubwa ya watu maskini, kila leo kunawasababishia maafa makubwa wananchi wa nchi hiyo. Hata hivyo tajiriba imethibitisha kwamba, mtu yeyote yule hawezi kufikia malengo yake ya kisiasa kwa kutumia mashambulizi ya kijeshi na kuua watu, bali matunda pekee ya hatua kama hizo ni kuzidisha mgogoro na kueneza chuki na ukosefu wa usalama.

Saudia inafanya mashambulizi ya kiholela bila ya kujali huko Yemen

 

Amma suala muhimu zaidi hapa ni kwamba, licha ya maonyo yanayotolewa mara kwa mara na mashirika ya kimataifa pamoja na watu muhimu duniani akiwemo Jan Egeland, kiongozi rasmi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu aliyelilaumu Baraza la Usalama la umoja huo kwa kuidharau na kuitelekeza Yemen, lakini umoja huo hadi hivi sasa umeshindwa kuchukua hatua yoyote ya maana ya kuwaokoa wananchi wanaoteketezwa na Saudia katika nchi hiyo ya Kiarabu. Hapa tunaweza kusema kuwa, Umoja wa Mataifa ni katika vyombo vilivyoonesha udhaifu mkubwa sana katika muongo wa hivi karibuni.

Kitendo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kuudharau mgogoro wa Yemen kimepandisha kiburi cha Saudi Arabia cha kushadidisha jinai zake dhidi ya Yemen bila ya soni wala kiwewe. Hata hivyo, Saudia imeshindwa kufikia malengo yake nchini Yemen na hilo linawapandisha hasira viongozi wa Riyadh na kuwapelekea kufanya jinai za kinyama zaidi ili kuficha aibu ya kushindwa kwao. Jambo hilo lakini linazidi kuamsha hisia za walimwengu ambao kadiri siku zinavyopita wanazidi kuonesha uungaji mkono wao kwa wananchi madhlumu wa Yemen na hasira zao kwa wavamizi wa nchi hiyo ya Kiarabu.