Mauritania yataka migogoro ya ulimwengu wa Kiislamu itatuliwe kisiasa
Rais Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania ametaka jitihada zaidi zifanyike za kuitafutia ufumbuzi wa kisiasa migogoro ya nchi za Kiarabu na Kiislamu
Rais Abdel Aziz amesema hayo katika kikao cha 28 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Jordan na kuongeza kuwa, magenge ya kigaidi yanazidi kupata nguvu katika baadhi ya nchi za Kiarabu na hivyo kuhatarisha usalama wa nchi hizo na utulivu wa kimataifa.
Vile vile Rais wa Mauritania ametaka kuundwa nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Quds Tukufu na kwamba njia pekee bora ya kuleta amani na usalama wa kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati, ni kupewa haki zao Wapalestina.
Wakati huo huo Abdul Qadir bin Saleh, Spika wa Bunge la Algeria amesema katika hotuba yake kwenye kikao cha 28 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwamba kuna ulazima wa kuangaliwa upya muundo wa jumuiya hiyo na kuongezwa kiwango cha ushirikiano baina ya nchi za Kiarabu.
Kwa upande wake, Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri alisema katika kikao hicho jana Jumatano kwamba, nchi yake inaunga mkono juhudi za kuitafutia utatuzi wa kisiasa migogoro ya Yemen, Syria, Iraq na Libya.
Amesema, Misri inaunga mkono utatuzi wa kisiasa wa Yemen kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa na kuzitaka nchi za Ghuba ya Uajemi kushirikiana katika utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo.
Kikao cha 28 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilifanyika jana Jumatano katika eneo la Bahrul Mayyit, nchini Jordan.