Michel Aoun: Ni mapema sana Arab League kuiita 'Ushirikiano wa Kiarabu'
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27076-michel_aoun_ni_mapema_sana_arab_league_kuiita_'ushirikiano_wa_kiarabu'
Rais Michel Aoun wa Lebanon ameonyesha masikitiko yake makubwa kwa kutokuwepo ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya wajumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League kwa ajili ya kuondoa mizozo na matatizo ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Mar 30, 2017 23:37 UTC
  • Michel Aoun: Ni mapema sana Arab League kuiita 'Ushirikiano wa Kiarabu'

Rais Michel Aoun wa Lebanon ameonyesha masikitiko yake makubwa kwa kutokuwepo ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya wajumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League kwa ajili ya kuondoa mizozo na matatizo ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Aoun ameyasema hayo baada ya kurejea kutoka nchini Jordan alikokwenda kushiriki kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kuongeza kuwa, ni mapema sana kuiita jumuiya hiyo kwa jina la 'Ushirikiano wa Kiarabu.'

Rais Michel Aoun wa Lebanon

Katika kikao cha 28 cha viongozi wa Arab League nchini Jordan, Rais Michel Aoun alikosoa vikali undumilakuwili wa jumuiya hiyo kuhusiana na migogoro ya hivi sasa ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema kuwa, chombo hicho kinatakiwa kujiangalia upya kutokana na misimamo yake hasi juu ya umwagaji mkubwa wa damu unaoshuhudiwa katika eneo hili.

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League 

Aliongeza kuwa, Arab League haitakiwi iwe inaomba msaada kutoka nje ya eneo hili kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi za Kiarabu. Pia alikosoa vikali baadhi ya nchi za Kiarabu kwa kuhusika katika uchochezi wa vita sambamba na kuipuuza kadhia ya Palestina. Kikao cha 28 cha viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Arab League kilimalizika juzi Jumatano usiku nchini Jordan.