Mayahudi waandamana Quds kulaani ukaliaji wa mabavu wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27172-mayahudi_waandamana_quds_kulaani_ukaliaji_wa_mabavu_wa_palestina
Maelfu ya Mayahudi wamefanya maandamano katika eneo la Quds tukufu kulaani upanuzi wa vitongoji vya walowezi za Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
Apr 02, 2017 03:36 UTC
  • Mayahudi waandamana Quds kulaani ukaliaji wa mabavu wa Palestina

Maelfu ya Mayahudi wamefanya maandamano katika eneo la Quds tukufu kulaani upanuzi wa vitongoji vya walowezi za Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Maandamano hayo yalifanyika jana usiku katika eneo la Jaffa, huko Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu, ambapo waandamanaji wamelaani ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina kwa miongo mitano sasa.

Waandaaji wa maandamano hayo ikiwemo harakati ya Standing Together wamesema lengo la wao kuandamana ni kuikosoa Tel Aviv, kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina, licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalopinga ujenzi huo. 

Maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umepasisha ujenzi wa kitongoji kipya huko kaskazini mwa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan hatua ambayo inakinzana na matakwa ya jamii ya kimataifa na wakati huo huo inakiuka maazimio ya kimataifa. 

Wiki iliyopita, wanaharakati wanaounga mkono Palestina walifanya maandamano nje ya ukumbi kulikofanyika kongamano la lobi ya Kizayuni la Kamati ya Marekani na Israel ya Masuala ya Umma (AIPAC) mjini Washington, aghalabu yao wakiwa ni wanaharakati wa mrengo wa kushoto wa vuguvugu la Jewish Resistance.

Kadhalika Jumatano iliyopita, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilitoa taarifa ya kulaani ukaliaji wa mabavu ya ardhi za Palestina sambamba na kutoa wito wa kuundwa taifa huru la Palestina, mwito uliotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.