Wazayuni: Tumeshindwa kuisambaratisha Intifadha ya Quds
Duru za Wazayuni zinaripoti kwamba, utawala ghasibu wa Israel umeshindwa kukabiliana na Intifadha ya Quds inayoendeshwa na wanamapambano wa Kipalestina.
Ripoti zinaeleza kuwa, katika mazingira ya hivi sasa Israel haina uwezo wa kukabiliana na wanamapambano wa Kipalestina na hivyo kuisimamisha Intifadha ya Quds iliyoanza Oktoba mwaka jana. Ron Huldai Meya wa Tel Aviv ameashiria woga na wahaka wa Wazayuni na kukosa amani kunakowakabili Wazayuni kutokana na kuendelea operesheni za wanamapambano wa Kipalestina na kubainisha kwamba, ukweli wa mambo ni kuwa, imekuwa haiwezekani kukabiliana na wanamapambano hao kwani wamekuwa wakitekeleza operesheni zao kwa kushtukiza.
Wakati huo huo, Ben Caspit mchambuzi mahiri wa Israel ameashiria jinsi mashirika ya usalama ya Israel yalivyochanganyikiwa katika kutoa majibu kwa operesheni za wanamapambano wa Kipalestina na kusema kuwa, mashirika hayo hayana uwezo wa kutoa mikakati ya kuhitimisha au hata kupunguza operesheni hizo za Wapalestina.
Mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa wa Israel ameyabeza na kuyaponda matamshi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Yisrael Katz Waziri wa Usafiri na Barabara waliotaka kubaidishwa familia za watekelezaji wa operesheni za wanamapambano wa Kipalestina.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kuandamwa na kashfa mbalimbali za ufisadi na utovu wa maadili huku migogoro katika utawala huo ghasibu ikishadidi kila siku.