PLO: White House imekaliwa na kuendeshwa na Wazayuni
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imesema Ikulu ya Marekani ya White House imekaliwa na kuendeshwa na walowezi wa Kiyahudi.
Hanan Ashrawi, mwanachama wa Kamati Kuu ya PLO amesema sera za kuchupa mipaka za mrengo wa kulia ndizo zimetawala Ikulu ya White House.
Amesema: "Tumekuwa tukilalama namna sera za walowezi wa Kiyahudi zinavyowakandamiza, kuwabagua na kuwadhulumu Wapalestina, Waarabu na Waislamu, lakini kwa sasa tunaona wazi kwamba Mayahudi ndio wanaoiendesha Ikulu ya White House moja kwa moja."
Mwanachama huyo wa Kamati Kuu ya PLO amesema utawala wa Rais Donald Trump unatekeleza misimamo ya kufurutu ada kama ya Benjami Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Matamshi haya yametolewa katika hali ambayo, duru za habari zinasema kuwa ujumbe wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina unatazamiwa kuelekea Marekani mwishoni mwa mwezi huu, kujiandaa kwa mkutano kati ya Trump na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.