Wayemen watungua helikopta ya Saudia, askari kadhaa wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27956-wayemen_watungua_helikopta_ya_saudia_askari_kadhaa_wauawa
Jeshi la Yemen likishirikiana na wapiganaji wa kujitolea limefanikiwa kutungua helikopta ya kisasa ya Saudi Arabia ambayo ilikuwa ikitumika katika mashambulizi ya anga ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo jirani ya Kiarabu.
(last modified 2026-01-01T09:10:44+00:00 )
Apr 19, 2017 02:30 UTC
  • Wayemen watungua helikopta ya Saudia, askari kadhaa wauawa

Jeshi la Yemen likishirikiana na wapiganaji wa kujitolea limefanikiwa kutungua helikopta ya kisasa ya Saudi Arabia ambayo ilikuwa ikitumika katika mashambulizi ya anga ya Riyadh dhidi ya nchi hiyo jirani ya Kiarabu.

Duru za habari zinasema kuwa, helikopta hiyo aina ya Black Hawk ilitunguliwa hapo jana Jumanne na jeshi la Yemen katika mkoa wa Ma’rib, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo masikini inayokabiliwa na hujuma za kila leo za Aal-Saud.

Habari zaidi zinasema kuwa, yumkini askari na vibaraka 13 wa utawala wa kifalme wa Aal-Saud waliokuwemo kwenye helikopta hiyo wameangamizwa baada ya ndege hiyo kutunguliwa.

Licha ya kwamba Jeshi la Saudia limesema helikopta hiyo imetunguliwa baada ya kulengwa kimakosa na mfumo wa kuzuia makombora wa Umoja wa Falme za Kiarabu, lakini Wayemen wanasema helikopta hiyo ya Riyadh imelengwa kwa kombora la ardhini hadi angani na askari watiifu kwa harakati ya Houthi ambao walikuwa wanamuunga mkono Ali Abdullah Saleh, rais wa zamani wa Yemen.

Moja ya helikopta za Saudia katika anga ya Yemen

Hii ni katika hali ambayo, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Ansarullah, limeendelea kupata mafanikio katika operesheni kadhaa lilizozifanya katika mikoa ya Lahij, Dhale na Taiz na kufanikiwa kuwaangamiza askari wengi vibaraka wa Saudia sambamba na kuwatia hasara kubwa.

Utawala wa Aal-Saud kwa kushirikiana na Marekani, Uingereza, utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake Abdrabbuh Mansur Hadi.