Wazayuni waendelea kujenga vitongoji vya Wazayuni katika ardhi za Wapalestina
Licha ya dunia nzima kulalamikia vikali jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel za kupora ardhi za Wapalestina na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, lakini viongozi wa Israel wamepasisha mradi wa kujenga nyumba 212 za walowezi wa Kizayuni katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Baytul Muqaddas.
Redio ya jeshi la utawala wa Kizayuni ilitangaza habari hiyo jana (Jumatano) na kuongeza kuwa, meya wa utawala wa Kizayuni ameafiki kujengwa nyumba 212 katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mashariki mwa mji wa Quds, ikiwa ni kuendeleza miradi ya kupanua vitongoji vya walowezi hao katika ardhi wanazoporwa Wapalestina.
Hatua hiyo imechukuliwa wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni lilipasisha azimio la kulaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina. Ukitoa Marekani, azimio hilo lilipasishwa kwa kura mutlaki za wanachama wote wa baraza hilo.
Kwa mujibu wa azimio hilo, utawala wa Kizayuni wa Israel una wajibu wa kuacha mara moja miradi yake yote ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina huko Quds Mashariki.
Tangu mwanzoni mwa mwaka 2016, Israel ilishadidisha jinai zake za kupora ardhi za Wapalestina kiasi kwamba kiwango cha kuporwa ardhi za Wapalestina kimeongezeka kwa asilimia 439 mwaka huu huu ikilinganishwa na wakati kama huu mwaka jana.
Israel imeongeza kasi ya kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ili kuvuruga muundo wa kijiografia na kijamii wa miji na maeneo ya Wapalestina na hivyo kuzuia kikamilifu kuundwa nchi huru ya Palestina.