Assad: Magaidi wanapata himaya ya Marekani, wanatumia kila mbinu vitani Syria
Rais Bashar al Assad wa Syria amesema maadui wa taifa la Syria hasa magaidi wakufurishaji wanaopata himaya ya Marekani wanatumia kila mbinu katika vita vyao dhidi ya watu wa Syria.
Rais Assad aliyasema hayo Jumamosi mjini Damascus, katika kikao cha kamati kuu ya chama cha Ba'ath na kuongeza: "Maadamu magaidi wako katika ardhi ya Syria vita dhidi ya ugaidi vitaendelea."
Assad amesema atakabiliana na njama zote za kuvuruga mamlaka ya kujitawala na umoja wa kitaifa. Ameendelea kusema kuwa nchi za Magharibi hasa Marekani zinawuanga mkono magaidi ndani ya Syria na kwa njia hiyo kuifanya kazi ya jeshi la nchi hiyo kuwa ngumu zaidi.
Rais Assad pia ameashiria hujuma ya hivi karibuni ya Marekani katika uwanja wa ndege wa kijeshi wa Al Shayrat na kusema: "Hujuma hii ilitekelezwa baada ya magaidi kupata pigo kaskazini mwa Hama na kusonga mbele jeshi katika maeneo ya kaskazini na mashariki."

Ikumbukwe kuwa Ijumaa Aprili 7, Marekani kwa kutumia kisingizio cha hujuma yenye kutiliwa shaka ya silaha za kemikali Aprili nne mkoani Idlib ilivurumisha makombora 59 ya Tomahawk katika uwanja wa ndege wa Al Shayrat huko Homs magharibi mwa Syria.
Rais Assad amesema, sambamba na vita dhidi ya ugaidi, kunaendelezwa jitihada za kisiasa kwa ajili ya maelewano ya kitaifa na kuongeza kuwa serikali yake inashiriki katika mazungumzo ya kisiasa ya Geneva kwa ajili ya kuzuia umwagikaji zaidi wa damu ya watu wa Syria.