Juhudi za Saudia za kuishawishi Misri ijiunge na siasa zake
Mfalme Salaman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia na Rais Abdul Fattah al Sisi wamekuatana na kufanya mazungumzo ambayo yamehusu suala la kuboresha uhusiano wa pande mbili na matukio ya kikanda na kimataifa.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Misri imesema kuwa, safari ya Abdul Fattah al Sisi nchini Saudi Arabia imefanyika kwa lengo la kushauriana na viongozi wa Riyadh juu ya masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa hususan suala la kupambana na ugaidi.
Mfalme wa Saudia na Rais wa Misri walikuna pia tarehe 29 Machi pambizoni mwa mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliofanyika nchini Jordan.
Uhusiano wa Misri na Saudi Arabia uliingia doa baada ya Cairo kujitenga na siasa za Riyadh kuhusu kadhia ya Syria. Saudi Arabia ilikasirishwa sana na kura ya ndiyo ya Misri kwa muswada uliopendekezwa na Russia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Oktoba mwaka jana kuhusu kadhia ya Syria. Kura hiyo ya Misri ilivuruga zaidi uhusiano wake na serikali ya Riyadh na katika hatua ya kwanza kampuni ya mafuta ya Aramco ya Saudi Arabia ilisitisha upelekaji wa bidhaa zake nchini Misri.
Kabla ya hatua hiyo serikali ya al Sisi iliipatia Saudia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir lakini suala hilo lilikwamishwa na mahakama baada ya malalamiko na upinzani mkubwa wa wananchi. Kadhia hiyo imeendelea kuwa katika orodha ya hitilafu za pande hizo mbili. Kutojiunga moja kwa moja Misri na vita vya Saudia dhidi ya watu wa Yemen ni miongoni mwa masuala mengi yanayozusha hitilafu kati ya Cairo na Riyadh. Kabla ya safari ya Abdul Fattah al Sisi nchini Saudi Arabia, msemaji wa jeshi la Saudi Arabia Ahmad al Asiri alikuwa amedai kwamba, Rais Abdul Fattah al Sisi wa Misri ametoa amri ya kushiriki wanajeshi elfu 40 wa nchi hiyo katika vita vya nchi kavu huko Yemen. Hata hivyo masaa machache baadaye afisa mmoja wa serikali ya Misri alikabidhibisha madai hayo na kusema hayana msingi wowote. Afisa huyo alisisitiza kuwa, suala la kutuma jeshi la Misri kupigana nje ya nchi linahitaji sheria maalumu.
Mkutano na mazungumzo ya Mfalme Salman wa Saudi Arabia na Rais Abdul Fattah al Sisi mjini Riyadh baada ya viongozi hao kukutana yapata mwezi mmoja uliopita huko Jordan, ni ishara kwamba, Saudia inaihitajia Misri katika utekelezaji wa siasa na sera zake za kikanda. Misri inahesabiwa kuwa nchi muhimu katika ulimwengu wa Kiarabu, na Saudia inafanya jitihada za kuishawishi kujiunga na siasa zake za upande mmoja kuhusu masuala ya kieneo na kimataifa yakiwemo masuala ya Syria na Yemen.
Katika miaka ya hivi karibuni Saudi Arabia imefeli sana katika sera zake za kisiasa na kiuchumi na kwa msingi huo inahitajia ushirikiano wa nchi kama Misri ili kufufua na kuhuisha nafasi yake. Uvamizi na vita vya Yemen vimeifanya Riyadh ihitajie msaada wa nchi kadhaa za Kiarabu na kimagharibi. Kurefuka kwa vita hivyo, kinyume na makadirio ya awali ya serikali ya Riyadh, kumevuruga mahesabu ya Saudia na kuitumbukiza katika kinamasi ambacho sasa imekuwa vigumu kuondoka humo bila ya msaada wa nchi nyingine. Hivyo sambamba na jitihada hizo za Saudia za kupata washirika wapya katika vita vya Yemen, Marekani kwa upande wake imetangaza kuwa itaipatia Riyadh mfumo wa makombora ya kuongozwa kutoka mbali kwa ajili ya Yemen.
Pamoja na hayo yote na kwa kutilia maanani radiamali na upinzani wa Wamisri dhidi ya hatua ya upande mmoja ya Rais Abdul Fattah al Sisi ya kuipatia Saudia visiwa viwili vya Tiran na Sanafir, inaonekana kwamba haitakuwa rahisi kwa Misri kushiriki moja kwa moja katika vita vya Yemen. Baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Hosni Mubarak, watu wa Misri walipata tajiriba mpya na upeo mpana zaidi kuhusu masuala ya kisaisa na hapana shaka kuwa, hawatastahamili kuona nchi yao ikizifuata kibubusa nchi nyingine hususan Saudia katika vita vya umwagaji damu huko Yemen.