Kuongezeka malalamiko ya wananchi na wasiwasi wa watawala wa Saudi Arabia
-
Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa Saudi Arabia
Katika kipindi cha chini ya siku 10, vijana wa Saudi Arabia wametumia mitandao ya kijamii kutoa mwito mwingine wa maandamano ya kulalamikia hali mbaya ya kimaisha nchini mwao.
Jana Alkhamisi, mitandao ya kijamii ilienea mwito wa vijana wa Saudi Arabia wanaowataka wananchi wa nchi hiyo kushiriki katika maandamano makubwa ya watu wasio na ajira siku ya Jumapili ijayo ya tarehe 30 Aprili. Kiwango cha ukosefu wa kazi nchini Saudi Arabia kilipanda kwa zaidi ya asilimia 12 mwaka jana ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Malalamiko nchini Saudi Arabia hayaishii tu katika siku za hivi karibuni, ni mgogoro wa miaka mingi na yameshadidi katika kipindi kisichopungua miaka sita mfululizo sasa. Mtu anaweza kujiuliza, mbona malalamiko hayo huwa yanaenda yakizima na baadaye kuibuka tena? Wachambuzi wa mambo wanasema, kabla ya kufikiria kuwa sababu ya jambo hilo ni kutengenea hali za kimaisha ya wananchi au kuridhishwa kwao na serikali, inabidi kufikiria kwanza siasa za ukandamizaji zinazoendeshwa na serikali ya nchi hiyo za kuwanyamazisha wananchi.
Kwa mfano tarehe 21 Aprili yaani wiki moja iliyopita, wananchi wa Saudi Arabia walitaka kufanya maandamano ya kulalamikia hali yao mbaya ya kiuchumi hususan kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi, hata hivyo serikali ya Saudi Arabia ilimwaga idadi kubwa ya askari wake mjini Riyadh na kuzuia kabisa kufanyika maandamano hayo. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hata kama keshokutwa Jumapili, tarehe 30 Aprili, utawala wa Aal Saud utazuia tena kufanyika maandamano ya wananchi, lakini pamoja na hayo hatua hiyo nayo itakuwa ni tishio kwa serikali ya Saudi Arabia.
Tishio hilo lina vipengee viwili. Kipengee cha kwanza ni kwamba wananchi wa Saudi Arabia wameonesha kutoridhishwa kwao na hali yao ya kiuchumi hususan kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na kupungua sana marupurupu ya wafanyakazi. Mfalme wa Saudi Arabia alijua vyema hilo na ndio maana wiki iliyopita alitoa amri ya kifalme ya kurejeshwa marupurupu yote ya wafanyakazi wa umma na wa vikosi vya ulinzi. Marupurupu hayo yalikatwa baada ya kuporomoka vibaya bei ya mafuta katika soko la dunia na fedha kubwa zinazotumiwa na serikali ya Saudia nje ya nchi hiyo hususan baada ya ukoo wa Aal Saud kuanzisha vita dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Septemba 2016 vita ambavyo vinakula pesa nyingi sana za wananchi wa Saudia. Weledi wa mambo wanasema, hatua kama hiyo ya mfalme wa Saudia inaweza kutuliza kwa muda tu malalamiko ya baadhi ya wananchi wanaofanya kazi, lakini kiwango kikubwa cha wananchi wataendelea kulalamika hususan vijana wasio na kazi na hilo ni tishio kubwa kwa serikali ya Riyadh.
Upeo wa pili wa jambo hilo ni kwamba, wananchi wa Saudi Arabia hawafurahishi na siasa za ukoo wa Aal Saud za kuingilia mambo ya nchi nyingine na kusahau hali yao ya ndani kwani wanaamini kuwa fedha nyingi zinazotumika katika kuingilia mambo ya nchi nyingine ndiyo sababu kuu ya matatizo yao ya kiuchumi na kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi. Si hayo tu, lakini pia ukoo wa Aal Saud unalazimika kutumia fedha nyingi ili kuvutia uungaji mkono wa madola ya Magharibi. Ukoo huo unatumia mabilioni ya dola kununua silaha kutoka nchi za Magharibi. Ripoti ya hivi karibuni ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa usalama duniani yenye makao yake mjini Stockholm Sweden inaonesha kuwa, mwaka 2016 na licha ya Saudi Arabia kupunguza kwa asilimia 30 matumizi yake ya kijeshi ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake wa 2015, lakini pamoja na hayo ilitumia dola bilioni 63 na milioni 700 katika mambo ya kijeshi na ilikuwa nchi ya nne duniani kwa kutenga fedha nyingi zaidi katika masuala ya kijeshi.
Ijapokuwa serikali ya Saudi Arabia imeandaa mipango mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufukuza wafanyakazi wa kigeni, lakini jambo lisilo na shaka ni kwamba, kitu ambacho kinaweza kuukwamua ukoo wa Aal Saud katika hatari ya kuongezeka malalamiko ya wananchi hususan ya kiuchumi na kiwango kikubwa cha ukosefu wa kazi, ni kubadilisha siasa zake za kupenda vita na kuingilia masuala ya nchi nyingine na badala yake kufanya juhudi za kuimarisha usalama na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati.