Saudi yaipongeza Marekani kwa kuendeleza sera za uhasama dhidi ya Iran
Adel al Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, katika safari yake ya hivi karibuni nchini Marekani, alizungumza na waandishi habari na kusema, safari ijayo ya rais Trump wa Marekani nchini Saudia itakuwa ya kihistoria huku akimpongeza rais huyo na serikali yake kwa misimamo yao mikali na ya uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Adel al Jubeir aliongeza kuwa: "Kwa mtazamo wangu serikali ya Marekani imechukua hatua za kwanza kuifahamisha Iran kuwa inapaswa kubadilisha mwenendo wake."
Trump ameichagua Saudi Arabia kama nchi ya kwanza ya kigeni kuitembelea tokea aingie madarakani mwezi Januari mwaka huu. Safari ya Trump katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, inatazamiwa kuanza tarehe 23 mwezi huu wa Mei.
Kwa mtazamo wa Saudia safari hii itakuwa ni nukta muhimu katika uhusiano wa Washington an Riyadh lakini tunapaswa kusubiri kuona hanimoni hii ya Marekani ya Trump na Saudi Arabia itadumu hadi lini.
Matamshi ya Adel al Jubeir kuhusu safari hiii inaashiria mhemuko kupita kiasi walionao watawala wa Saudia.
Al Jubeir anatumia mazingira yaliyopo katika uhusuano wa nchi yake na Marekani kujaribu kuonyesha kuwa safari ya Trump ina maana ya kuunga mkono kikamilifu sera za Saudia.
Hii ni katika hali ambayo, fikra za misimamo mikali za Kiwahabi ambazo zinaenezwa na watawala wa Saudia ndio chanzo kikuu cha kuenea ugaidi na magaidi duniani.
Kwa maneneo mengine ni kuwa, Saudia kimsingi haina nia wala azma imara ya kupambana na ugaidi; kama ambavyo Marekani nayo pia haijawahi kuwa na nia ya kuangamiza ugaidi. Kwa msingi huo tunaweza pia kuutazama uhusiano wa Marekani na Saudia kwa darubini hiyo.
Baada ya kutembelea Riyadh, Trump ataelekea Tel Aviv. Kwa hivyo kwa kutembelea miji hiyo miwili, inabainika wazi kuwa serikali mpya ya Marekani imeelekeza sera zake katika eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu.
Kuna sababu kadhaa ambazo zimempelekea Trump kulipatia umuhimu suala la uhusiano na Saudi Arabia. La muhimu kabisa ni uuzaji silaha na kutumia kwa maslahi yake changamoto za kiusalama ilizonazo Saudia katika eneo. Katika kufikia malengo yake ya kutafuta soko la silaha zake, Marekani inalenga kuunda muungano mpya wa kiijeshi Mashariki ya Kati chini ya uongozi wa Saudia. Ni kwa sababu hiyo ndio katika safari yake Saudia, Trump hatakutana tu na wakuu wa nchi hiyo bali pia wafalme wa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi wametakiwa kufika mjini Riyadh ili wakutane na rais huyo wa Marekani.
Kwa hivyo Trump atafuatilia malengo kadhaa katika safari yake hiyo. Hivi sasa Marekani inafuatilia kwa karibu suala la kutaka Iran itengwe katika eneo. Saudi Arabia nayo pia inafuatilia sera hiyo hiyo ya kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo. Hii ndio sababu watawala wa Saudia wakachochea na kushadidisha vita katika nchi kama vile Syria, Yemen, Iraq na Palestina. Pamoja na hayo tunapaswa kusubiri kuona uchochezi huo wa Saudia utafika wapi.
Kile kilicho wazi ni kuwa, sera za Marekani zimejengeka katika msingi wa kufuatilia maslahi ya Washington katika eneo. Lakini la kusikitisha ni kuwa aghalabu ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudia yenyewe zinatumia vibaya na kwa ubadhirifu mabilioni ya dola ya pato lao la uuzaji mafuta ya petroli kununulia silaha. Nchi hizo zinatumia pato hilo la mafuta kununua idadi kubwa ya silaha kutoka nchi za Magharibi pasina kuzingatia umuhimu wa nchi za Kiislamu kuungana na kuwa na mshikamano wa kisiasa na kijeshi.
Natija pekee ya sera hizo ni kushiriki Saudia na Marekani katika vita vya kulazimishwa katika baadhi ya nchi za Kiislamu sambamba na kuudhaminia usalama utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina na nchi zingine za Kiarabu.
Kilicho wazi ni kuwa katika sera zake za Mashariki ya Kati, Marekani imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Saudi Arabia pamoja na utawala haramu wa Israel na mkondo huo ungali unaendelea.