Hania asifu juhudi za mateka wa Kipalestina za kukomboa Palestina
Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesifu juhudi za mateka wa Kipalestina za kukomboa ardhi za Palestina na kusisitiza kwamba, kamwe Hamas na wananchi wa taifa hilo madhulumu hawatawasahau.
Ismail Hania amesema hayo mjini Gaza ambapo akiwahutubu mateka wa Kipalestina wanaogoma kula katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel amesema kuwa, wafungwa mashujaa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israel wanapaswa kutambua kwamba, Hamas na wananchi wa Palestina katu hawatawasahau na wala hawatafumbia macho haki zao na kuwa wataendelea na harakati zao kuhakikisha kwamba, mateka wote wanaoshikiliwa katika magereza ya Wazayuni maghasibu wanaachiliwa huru.
Amesema kuwa, mapambano ya mateka wa Palestina katika jela za Israel ni mapambano ya Wapalestina wote na kuwa, mapambano ya ukombozi wa Palestina yanasonga mbele tena kwa nguvu na kasi kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Tangu tarehe 17 ya mwezi uliopita wa Aprili zaidi ya Wapalestina 1,700 wanaoshikiliwa kwenye jela za utawala haramu wa Israel walianzisha mgomo usio na muda maalum wa kususia chakula kulalamikia vitendo vya ukatili na vya kinyama pamoja na hali mbaya ya huduma na mazingira inayowakabili katika jela hizo.
Kituo cha utafiiti kuhusu mateka wa Kipalestina kimetangaza kuwa hivi sasa kuna Wapalestina wapatao elfu saba wanaoishi katika hali mbaya ya kibinadamu kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.